RAIS MAGUFULI AAGIZA MACHINGA WASISUMBULIWE.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu
katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara
moja utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina
la Machinga katika Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka
husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa
kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli
akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo tarehe
06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote
ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.
"Kumeibuka tabia
ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila
utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya
mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, wakati mwingine wanawafukuza
wachimbaji wadogo kwenye maeneo wanayofanya shughuli zao na pia wanawafukuza
wafugaji katika maeneo wanayolisha mifugo yao, hili sio sawa.
"Sipendi
Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria
katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi
kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana
yake tunaanza kutengeneza madaraja ya
Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa
katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya
mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze
madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini,
sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho"
amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli
ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo yao Jijini Mwanza waachwe
waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza
itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha
Wamachinga wenyewe.
"Narudia na
hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye
maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa
na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu
yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha
viongozi wa Wamachinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia
hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo,
nadhani mmenielewa" amesisitiza Rais
Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na
Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na
Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji
cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala
yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji
anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.
"Wale
waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji
ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini,
waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha
watoto wao lakini wanafukuzwa tu.
"Na hizi ndio
ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda
kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini"
amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli
amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo
wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa kutengeneza nyaraka zinaonesha
mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza
kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Hata hivyo Rais
Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo
waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka
zisiwanyanyase watu wanyonge
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
06 Desemba,
2016
Tazama Video hapa chini kumsikia akizungumzia suala hilo;
Post a Comment