Freemasons Tanzania wapata pigo, Sir Andy Chande Afariki Dunia
Aliyekuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Tanzania na Afrika Mashariki, Sir Jayantilal Keshavji ‘Andy’ Chande, amefariki dunia.
Sir Chande amekuwa mwanachama wa Freemason kwa takribani miongo sita tangu ajiunge na umoja huo mwaka 1954.
Kiongozi huyo alizaliwa Mombasa, Kenya Mei 7, 1928 ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene Mjini mkoani Tabora.
Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana asubuhi.
Kulingana na taarifa hizo, kiongozi huyo alifariki dunia jijini Nairobi, Kenya alikokuwa akitibiwa.
Kiongozi huyo aliwahi kueleza kuwa alijiunga na Freemason Oktoba 25 mwaka 1954 baada ya kupitia usaili.
Aliwahi pia kutunga kitabu alichokiita kwa jina la ‘A night in Africa –journey from Bukene’ (usiku wa Afrika – safari kutoka Bukene).
Katika miaka ya 1950 ndipo alieleza kuanza kutambua kuwa Freemason ipo katika msingi wake, ikiwa ni pamoja na sayansi ya maisha ambayo malengo yake ni kumbadilisha mtu kiimani na kumfanya awe anavyopaswa kuwa.
Aliwahi kuelezea kanuni tatu kubwa za Freemason ikiwa ni pamoja na kumtaka mtu kuwa mkweli na mwenye maadili ambayo hasa Freemason inalenga kuyaweka kwenye akili ili mwanachama awe mzuri.
Ngazi ya pili ya utaratibu inatilia mkazo kwenye vipaji na akili kupitia sanaa na sayansi ili kutoa mchango mzuri iwezekanavyo katika maisha.
Ngazi ya tatu alisema kuwa unafundishwa namna ya kufurahia maisha kwa kiwango chake cha juu kwa kufuata kanuni hizo na mwisho ni upendo wa kindugu, kujiweka huru na ukweli.
Katika masha yake aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Shaaban Robert.
Akiwa kwenye Jumuiya ya Freemason katika uhai wake, Sir Chande aliwahi pia kukutana na viongozi mashuhuri nchini kama vile Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, marais wastaafu, Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Hata hivyo kutokana na fikra zilizojengeka katika jamii, Freemason ilikuwa ikiogopwa na kutajwa tajwa na watu vibaya, mojawapo ikiwa ni kupata utajiri kwa njia isiyo ya kawaida.
Hata hivyo, hadi sasa dhana hiyo inaendelea na hakuna lililo wazi katika hili, huku katika mitandao ya kijamii kila mmoja akijadili jumuiya hiyo kadiri anavyoifahamu au kuisikia.
Histora yake
Sir Chande alizaliwa Mombasa, Kenya Mei 7, 1928, ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania.
Alifika Tanzania mwaka 1950, alihamia Dar es salaam 1953 na kukutana na watu wengi wa bandarini, shirika la reli na mashirika mbalimbali aliyofanyia kazi.
Katika simulizi zake kadhaa, Sir Chande alisema alikutana na watu wengi ambao walikuwa wanahudhuria vikao vya Freemason, akaanza kuulizia na akajifunza mambo kadhaa kuhusu watu hao.
Wakati huo, hao watu hawakuwa huru kuzungumzia Freemason kama alivyofanya Sir Chande, hasa kabla ya vita ya pili ya dunia.
Sir Chande alisema wakati huo Freemason ilikuwa imegawanywa makundi tofauti, katika hospitali, shule, na mashirika mbalimbali na kulikuwa na kundi maalumu kwa ajili ya matajiri na wafanyakazi wakubwa wa Serikali. Ukiangalia vizuri wengi wao walikuwa ni wazungu na baadhi ya Wahindi.
Kundi la kwanza lilikuwa linaongozwa na watu wa Scotland, makundi mawili yaliyofuata yalikuwa yanaongozwa na Waingereza na kundi la nne lilikuwa linaongozwa na Wahindi ambalo ndilo Chande alilojiunga nalo. Ilimchukua miaka miwili kukubaliwa kujiunga na Freemason.
Aliapishwa rasmi mwaka 1954 akiwa na umri wa miaka 28. Kumbuka kwamba masharti ya kujiunga ni lazima uwe na umri kuanzia miaka 21.
Baada ya hapo ndipo alipanda cheo na kupewa nafasi ya kuongoza kundi au tawi la Freemason katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.
Akajiunga na miradi tofauti ya Freemason nchini Uingereza yakiwemo hoteli za kifahari pamoja na kupewa jukumu la kujenga hoteli mpya ya Freemason nchini Ghana kwenye Mji wa Khumasi ambayo ni ya kifahari.
Hoteli nyingine ya kifahari aliyoisimamia ujenzi wake iko Zambia.
Sir Chande anakumbukwa sana kwa kuanzisha shule ya msingi ya Viziwi Buguruni, Dar es Salaam, moja ya taasisi ambazo alizipa kipaumbele mno hadi anaingia kaburini.
Sir Andy Chande alistaafu kama kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki mwaka 2005 baada ya kuifanyia kazi kwa miaka 19, akawa hahudhurii mikutano ya nchi hizi, lakini akishiriki ile ya Uingereza kwa sababu alikuwa akiendelea kufanya kazi na mashirika ya huko.
Freemason ni nini?
Freemason ni taasisi kongwe, kubwa na inayotambulika kote duniani.
Pamoja na kwamba shirika hili katika muundo wake wa sasa lilianzishwa mjini London, Uingereza mwaka 1717, lakini historia yake inaelezwa kurudi nyuma katika karne ya 14.
Limekuwa likitajwa kwa kila aina ya minong’ono kiasi kuwa baadhi ya matapeli wamekuwa wakiitumia fursa hiyo kujinufaisha, ikiwamo kutoa matangazo ya kualika watu kujiunga wakilenga kukusanya fedha za ada kwa minajili ya kuwafanya wanachama hao tarajiwa kuwa tajiri, wenye nguvu na ushawishi.
Licha ya marehemu Chande na viongozi wengine duniani kuizungumzia kwa uzuri, lakini bado Freemason inabakia fumbo tata miongoni mwa watu wengi duniani wakiwamo Watanzania.
Kwa mujibu ya vitabu vya historia, Freemason kama neno linavyojieleza kwa Kiingereza, awali lilikuwa kundi la mafundi waashi (masons) au wajenzi kwa maneno mengine.
Walikuwa wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa mahekalu na mabenki katika zama za kati.
Mejengo mengi ya kale kama vile makanisa, mji wa Rome, Washington DC ilisanifiwa na kujengwa na mafundi hawa ndiyo maana mengi yna alama zao.
Lakini pia vitabu vya historia vinaeleza waashi hawa kutokana na uaminifu wao, walikabidhiwa masuala ya utunzaji fedha za asasi mbalimbali kubwa hasa benki na Kanisa Katoliki.
Wakati wakijenga mahekalu, pia walitengeneza mahandaki ya kuhifadhi fedha na kuzikia.
Utaalamu wao wa ujenzi ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ukiingia ndani ya hayo mahandaki bila ramani unaweza kupotelea humo ndani usiweze kutoka tena.
Kwa sababu ya kuwa waashi, alama zao kubwa ni vifaa vya ujenzi kama vile pima maji.
Ikatokea kipindi ambapo hawa Freemason wanadaiwa kuasi na kuanza kujishirikisha na mambo ya nguvu za giza, utoaji kafara watu na ushirika na shetani.
Wengine wanasema walianza kuiba fedha za Kanisa Katoliki, lakini ukweli halisi haujulikani.
Kutokana na sababu hizi na nyingine ambazo ni siri kati ya Kanisa na Freemason, wakafukuzwa kutoka ukatoliki.
Ndiyo sababu ambayo inaelezwa kutokuwapo kwa maelewano kati yao na Wakatoliki pamoja na imani nyingine duniani.
Wakatoliki walianzisha shirika jingine badala ya Freemason lijulikanalo kama Jesuits.
Hata hivyo, Freemason ya sasa inaelezwa tofauti na viongozi wake wengi duniani, akiwamo marehemu Sir Chande.
Inajieleza kama taasisi ya kirafiki na kifamilia inayounganisha wanaume wenye tabia nzuri wa dini tofauti, wenye kuchangia imani moja katika ubaba wa Mungu na undugu duniani.
Utamaduni wa Freemason unaanzia wakati wa ujenzi wa hekalu la Mfalme Solomon na sherehe zake za kirafiki hutumia kazi za uashi kuashiria somo la maadili na ukweli.
Uanachama wa Freemason hauingiliani na imani ya mtu, familia au ajira yake na hivyo ni kundi lisilo la kidini wala kisiasa ambalo linakaribisha watu wa imani zote kwa malengo ya kuleta ustawi katika jamii.
Katika miaka ya 1990, Freemason ilipata changamoto kubwa nchini Kenya baada ya Rais, Daniel arap Moi kuunda tume kuchunguza watu wanaoabudu shetani, ambayo moja ya majukumu ya tume yalikuwa kuichunguza Freemason.
“Nilifika mbele ya tume hiyo mara mbili na katika nyakati tofauti kama Mkuu wa Freemason Afrika Mashariki. Nilitoa ushahidi kuhusu kazi tunazozifanya,” alikaririwa Sir Chande akisema wakati huo.
Ijapokuwa tume hiyo haikutoa majibu ya kazi waliyokabidhiwa na Rais Moi, inasemekana ilisafisha tuhuma zilizoelekezwa kwa Freemason.
“Nafurahi kusema kwamba tuhuma zile zilisafishwa zaidi na Rais aliyefuata baadaye, Mwai Kibaki ambaye katika moja ya hotuba zake, alisema Freemason imetoa mchango mkubwa sana nchini Kenya,” Sir Chande aliwahi kukaririwa akisema.
Akiwa na Diamond Platnumz
Akiwa na JM Kikwete
Akiwa na BW Mkapa
Akiwa na A.H. Mwinyi
Akiwa na JK Nyerere
Akiwa na Wanajumuiya wenzake wa Freemasonry
Post a Comment