Header Ads

Maelfu kushuhudia jeneza la Malkia likisafirishwa kwenda Edinburgh

 




CHANZO: BBCSWAHILI | C&P Safari ya mwisho na ya simanzi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza, imeanza mchana huu ambapo jeneza lake linasafirishwa kutoka Balmoral kupelekwa kwenye kasri la kifalme la Holyroodhouse huko Edinburgh.

Maelfu ya watu wanatarajia kupanga mstari kando kando ya barabara wakati mwili huo utakapokuwa unasafirishwa.

Hiyo ni hatua ya kwanza ya safari ya maziko yake yatakayofanyika wiki ijayo jijini London.

Mwili utaondoka Balmoral majira ya saa 7 mchana , na utasafirishwa taratibu kwa njia ya barabara kuelekea Edinburgh umbali wa takribani maili 175 sawa na 280km.

Utapitishwa katika maeneo tofauti kuanzia Aberdeen, Dundee, na Perth, na itakuwa safari ya karibu masaa 6.

Utawasili katika Jumba la Holyroodhouse - makazi rasmi ya mfalme wa Uingereza katika mji mkuu wa Scotland - na utahifadhiwa katika chumba maalumu.

Jumatatu alasiri, kutakuwa na huduma chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Giles, itakayohudhuriwa na watu wa Familia ya Kifalme. Jeneza hilo litakaa hapo kwa saa 24, kwa ajili ya watu kutoa heshima zao za mwisho. Siku inayofuata, Bintimfalme Anne ataandamana na mwili wa mama yake wakati ukisafirishwa kurejea London. Jeneza la Malkia litachukuliwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Edinburgh hadi Kasri la Buckingham kupitia RAF Northolt.

Je mazishi ya Malkia yanafanyika lini?

Maziko ya kitaifa ya Malkia Elizabeth yatafanyika Jumatatu ya Septemba 19, 2022 huko Westminster Abbey, kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Kasri la Buckingham.

Abbey ni Kanisa la kihistoria ambapo wafalme na malkia wa Uingereza wanatawazwa, ikiwa ni pamoja na kutawazwa kwa Malkia mnamo 1953, na ambapo aliolewa na Prince Philip mnamo 1947.


Hakujakuwa na ibada ya mazishi ya mfalme katika kanisa la Abbey tangu Karne ya 18, ingawa mazishi ya mamake Malkia yalifanyika huko mnamo 2002.

Wakuu wa nchi kutoka kote ulimwenguni watakuwa wakisafiri kwa ndege kuungana na washiriki wa Familia ya Kifalme kukumbuka maisha na huduma ya Malkia.

Wanasiasa wakuu wa Uingereza na mawaziri wakuu wa zamani pia watakuwepo.Siku itaanza huku jeneza la Malkia likibebwa kutoka Ukumbi wa Westminster hadi eneo la Westminster Abbey kwenye Gari la Jeshi la Wanamaji la Kifalme.

No comments