Rugemalira Asaka Dhamana Mahakama ya Rufaa
Mshitakiwa wa Kesi ya uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, James Rugemalira amewasilisha maombi matatu katika Mahakama ya Rufaa ikiwemo ombi la kusudio la kukata rufaa kupinga kunyimwa dhamana na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’.
Ombi lingine ni la kuitaka Mahakama hiyo kumuingiza katika maombi hayo, Mtuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, Habinder Sethi ambapo Rugemalira ameiomba Mahakama imuingize Sethi kama mtu muhimu katika kesi hiyo.
Maombi hayo yamewasilishwa jana Machi 5, 2018 mahakamani hapo na Rugemalira mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Benard Luanda na Jaji Gerald Ndika.
Hata hivyo, kulikuwa na mvutano kati ya upande wa Jamhuri na upande wa mshtakiwa baada ya Jamhuri kuweka pingamizi kwa kuiomba Mahakama ya Rufaa kuyatupilia mbali maombi hayo kwa madai kuwa, muwasilishaji alitumia kanuni zisizo sahihi huku upande wa utetezi ukipinga pingamizi hilo kwa madai kwamba Jamhuri haikuwasilisha pingamizi hilo kwa maandishi.
Kufuatia mvutano huo, Jaji Luanda amesema wanaahirisha maombi hayo na watapanga tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Post a Comment