Vipimo Vyakwamisha Kesi ya Nabii Tito
KESI inayomkabili mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma Tito Machibya, maarufu kama ‘Nabii Tito’ (45), ya kujaribu kujiua kwa kutumia wembe, imeahirishwa tena kuanza kusikilizwa hadi Machi 19, mwaka huu kutokana na ripoti ya vipimo vya akili kutokamilika.
Akiahirisha kesi hiyo jana, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Mwajuma Lukindo, alisema kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe hiyo kutokana na ripoti ya vipimo hivyo kutokamilika.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe Isanga kwa kawaida ripoti ya vipimo huchukua siku 42, hivyo kutokana na hali hiyo vipimo vya nabii huyo havijakamilika.
Februari 5, mwaka huu mahakama hiyo iliagiza kutekelezwa kwa amri iliyotolewa na Mahakama hiyo ambayo iliamuru jana, kupelekwa kwa vielelezo vinavyoonyesha Nabii Tito ana matatizo ya akili na kufanyiwa vipimo katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe Isanga.
Akitoa maelezo ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuwasilishwa kwa taarifa kutoka Isanga.
Hata hivyo, Hakimu Karayemaha alisema mshtakiwa huyo amewasilisha vielelezo vyake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na mahakama inahitaji taarifa kutoka Taasisi ya Mirembe Isanga kama ilivyoagiza.
“Mahakama ilitoa amri apelekwe Taasisi ya Mirembe Isanga kwa mujibu wa kifungu namba 219 (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,” alisema Hakimu Karayemaha.
Kifungu hicho kinasema kama mshtakiwa atabainika kuwa kweli ana matatizo ya afya ya akili, mahakama itaamua kuwa alivyofanya tukio hilo hakuwa na akili timamu, hivyo hana hatia.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Karayemaha alimuamuru Mkuu wa Magereza ya Isanga kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa ya kumpeleka kufanyiwa vipimo mshtakiwa huyo.
“Namuamuru Mkuu wa Magereza Isanga atekeleze amri ya mahakama, ili taarifa za mshtakiwa ziletwe Machi 5, mwaka huu, tutataja kesi na kupokea taarifa ya vielelezo vya vipimo vyake kutoka Isanga na mshtakiwa ataendelea kukaa rumande,” alisema hakimu huyo.
Nabii Tito anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu katika mtaa huo wa Ng’ong’ona.
Post a Comment