Mkurugenzi wa halmashauri ya msalala , Simon Berege akizungumza na wananchi baada ya ufunguzi wa maktaba ya shule ya sekondary ya Bulyanhulu.
Mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu umezindua na kukabidhi maktaba iliyogharimu shilingi milioni 22.6 kwenye shule ya sekondari Bulyang'hulu iliyopo katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kusaidia wanafunzi na walimu katika kuboresha ubora wa elimu inayotolewa.
Maktaba hiyo imezinduliwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Msalala Bw , Simon Berege na kuhudhuriwa na kaimu Meneja mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu,Elias Kasitila.
Akizungumza wakati uzinduzi huo, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi Bulyanhulu,Elias Kasitila alisema wakati wakitafakari namna ya kuinua taaluma ya wanafunzi waliona ni vyema wakaimarisha usomaji wa wanafunzi kwa kuwekeza kwenye maktaba ambayo itasaidia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi kutoka kwa jamii inayouzunguka mgodi huo.
Alisema kupitia mpango wa Acacia wa maendeleo ya jamii wameamua kushirikiana na shirika la kimataifa la Read International kuboresha jengo moja la shule hiyo na kuliwekea samani kwa ajili ya matumizi ya maktaba ambayo itawasaidia wanafunzi na walimu kwa kiasi kikubwa.
“Misaada inayotolewa na Acacia katika sekta ya elimu ni sehemu ya sera ya wajibikaji kwa jamii ya kampuni inayojikita katika kuhakikisha jamii inakuwa endelevu kupitia sekta ya elimu na sera hiyo inachangia moja kwa moja maono ya taifa hadi kufikia mwaka 2025 na malengo ya nchi ya kuleta maendeleo endelevu kwa kuhakikisha jamii inapata elimu iliyo bora”,alisema Kasitila.
Mwakilishi wa shirika la Read International linalojihusisha na masuala ya elimu,Esther Kalwinzi alisema pesa ambazo zimetolewa na mgodi huo ni shilingi milioni 22.6 kwa ajili kukarabati darasa kuwa maktaba.
Kwa upande wake,mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkurugenzi wa Halmashauri ya msalala , Simon Berege umeushukuru mgodi huo pamoja na shirika la Read International kwa kufadhili maktaba hiyo ya kisasa kwenye shule hiyo na kwamba itasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kujisomea na kujenga uwezo mkubwa kwenye masomo yao.
Kikubwa zaidi ninacho wasisitiza wanafunzi kuzingatia masomo na pia wazazi tambueni elimu ndiyo urithi pekee wa kudumu na wenye kubadilisha maisha ya mtoto kutoka hali ya chini ya umasikini kuja juu zaidi kimaisha”Alisisitiza Berege.
Hata hivyo mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Mussa Rajabu alisema kuzinduliwa kwa maktaba hiyo kutaleta chachu ya kupenda kujisomea zaidi na kwamba itawasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
|
Post a Comment