Mtuhumiwa wa Richmond Aachiwa Huru
Aliyekuwa Wakala wa Kampuni inayodaiwa kuwa ni kampuni hewa ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development LLC, Naeem Gire ameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Akitoa uamuzi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka mawili ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Uamuzi huo ni wa pili kutolewa na mahakama hiyo dhidi ya mashitaka yaliyokuwa yakimkabili Gire. Awali, aliachiwa huru baada ya kuonekana hana kesi ya kujibu, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa Mahakama Kuu.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilisema haikuwa sahihi kumwachia, kabla hajajitetea katika mashitaka ya kwanza na ya pili, ambayo ni kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo. Hivyo, kesi hiyo ilirejeshwa Mahakama ya Kisutu, na Gire akapanda tena kizimbani akajitetea na Hakimu Mkeha ametoa uamuzi huo.
Katika kesi hiyo hiyo, Julai 28, 2011 Gire aliachiwa huru katika mahakama hiyo na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema kuwa hana kesi ya kujibu, lakini Mahakama Kuu ilimtaka apande kizimbani tena kwa ajili ya kujitetea.
Katika uamuzi wake wa kumwachia huru Gire, Hakimu Lema alisema kuwa ameridhika na hoja za utetezi kuwa mshtakiwa huyo hana kesi ya kujibu, kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutengeneza kesi dhidhi ya mshtakiwa kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, kiasi cha kumlazimu ajitetee.
Hakimu Lema alisema baada ya kuupitia ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wa upande wa mashtaka , hoja za pande zote na vifungu vya sharia, aliridhika kuwa ushahidi huo hauna vigezo vya kuonesha kuwa mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu.
Uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa na Jaji Lawrence Kaduri katika rufaa ya DPP aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, kumwachia huru kuwa hana kesi ya kujibu.
Jaji Kaduri alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, ameridhika kuwa mshtakiwa huyo alikuwa na kesi ya kujibu na kwamba ushahidi huo unamlazimisha apande kizimbani kujitetea.
Hata hivyo, aliamuru mshtakiwa huyo arudi kizimbani katika Mahakama ya Kisutu ili aanze kujitetea na kwamba kesi hiyo isikilizwe na hakimu mwingine.
Post a Comment