Mgogo CUF Wazidi Kuwaka Moto......Wabunge Walaani, Polisi Wafuta Mkutano wa Maalim Seif
Siku moja baada ya kutokea kwa vurugu kubwa katika mkutano wa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa kuvamiwa na genge la watu waliokuwa na silaha za moto, wabunge wa upinzani wameibuka na kuitupia lawama Serikali.
Kutokana na hali hiyo wabunge hao wamesema ukimya wa Serikali kuhusu uvamizi huo wa viongozi wa CUF, huku wakitangaza kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Naibu Mnadhimu wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Ally Saleh alishangazwa na ukimya wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kwa kushindwa kujitokeza na kukemea hatua ya waandishi wa habari kupigwa katika mkutano huo.
Kutokana na hilo, wamelaani kitendo hicho cha uvamizi wa mkutano pamoja na waandishi wa habari kupigwa huku wakiitaka Serikali kutoa tamko na kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
Wakati wabunge hao wakitoa tamko hilo, Dk. Mwakyembe yeye amekana kuwa taarifa juu ya tukio hilo.
“Mimi sijui chochote ndiyo nasikia kwako, kwani hao wabunge wamekwambia kama wameniletea taarifa hizo? Mimi niko Dodoma…sifahamu chochote,” alisema.
Akizungumzia hali hiyo Saleh, alisema chama cha CUF, kimeshamwandikia barua IGP Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhusu tukio hilo.
Alisema ukimya wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Dk. Mwakyembe juu ya tukio hilo umeonesha kuwa hawajatimizi majukumu yao ipasavyo.
“Mambo haya yanavyotokea mawaziri wawili tunataka kuwavisha mnyororo, Waziri Mwigulu Nchemba na Mwakyembe.
“Mwakyembe alipaswa kujitokeza kwa haraka na kutoa tamko, tunahisi jukumu la Serikali halijatekelezwa, Mwakyembe anapaswa kuhakikisha usalama wa waandishi unakuwapo,” alisema.
Saleh ambaye ni Mbunge wa Malindi alisema kikundi cha ‘Mungiki’ si kigeni hapa nchini na Serikali inakifahamu lakini hakuna hatua zozote ambazo zimeshachukuliwa hadi sasa.
Aidha alisema kutokana na tukio lililotokea juzi, ziara iliyokuwa ifanywe na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad upande wa bara jana ilifutwa na Serikali.
“Kitendo cha Serikali kuufuta mkutano huo si sawa kwa sababu bwana yule (Profesa Ibrahim Lipumba) anabebwa na mbereko ya Serikali kwa kufanya mikutano ya ndani kila wakati.
“Serikali inalea Jamhuri ndogo ndani ya Jamhuri, vile vile Serikali imekuwa inalea kambi ndogo ndani ya Buguruni na kwamba wanufaika zaidi wa mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao dhumuni lao ni kuchukua majimbo yanayoongozwa na CUF katika uchaguzi mkuu ujao,”alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Devotha Minja alisema matukio wanayofanyiwa waandishi wa habari yanapaswa kukemewa.
“Waandishi wa habari ni kiungo cha serikali na wananchi, pia ni kiungo kati ya wanasiasa na wananchi, suala walilofanyiwa jana linapaswa kukemewa na halipaswi kuendelea kutokea,” alisema Minja.
Minja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema waandishi wa habari wamekuwa wakionewa na kupigwa, akitolea mfano wa tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds, kutekwa na kuteswa kwa Absalom Kibanda, kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daud Mwangosi.
Kutokana na vurugu hizo ambazo zilisababisha mtu mmija anayedaiwa kuvamia mkutano huo kujeruhiwa, Jeshi la Polisi limesema bado linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikilia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda, amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na wahusika waliosababisha vurugu hizo.
“ Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia jambo lolote kuhusu tukio hilo…tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu vurugu hizo na baada ya uchunguzi wetu kukamilika tutatoa taarifa ,”alisema Suzan.
Post a Comment