Header Ads

HOSPITALI ZOTE ZA MIKOA KUWA NA WATAALAM WA MIFUPA

 
WATAALAM wa mifupa wamepelekwa katika Hospitali zote za Kanda na matarajio ya baadaye ni kuwapeleka katika Hospitali za Mikoa ikiwa ni kusogeza huduma za tiba ya mifupa karibu zaidi na wananchi.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na kituo cha luninga cha TBC1 kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO jana jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ulisubisya amesema kuwa wataalamu hao wamepelekwa katika Hospitali hizo ili kutatua changamoto ya matibabu ya magonjwa ya mifupa yaliyoongezeka kwa wingi kutokana na ajali hasa zitokanazo na Bodaboda.

“Serikali imepeleka Wataalamu wa mifupa katika Hospitali za Kanda ikiwa ni njia ya kusogeza huduma za matibabu ya mifupa karibuzaidi na wananchi kwani kumekuwa na ongezeko la wagonjwa kutokana na ajali hasa za Bodaboda” amesema Dkt. Ulisubisya.

Aidha Katibu Mkuu huyo amesema kuwa pamoja na kupeleka wataalamu wa mifupa katika Hospitali za Kanda na mikoa, mikakati ya Serikali ni kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa bora na zinawafikia wananchi kwa urahisi ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuja na dhana ya kuwa na Zahanati kila Kijiji ambazo zitapatia dawa na vifaa tiba muhimu.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha dhana hiyo inatekelezeka Wizara ya Afya imekuwa ikishirikiana na TAMISEMI ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia huduma, kuhakikisha huduma za msingi zinapatikana ikiwemo miundombinu ya Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali pamoja na Dawa na Vifaa Tiba.

“Pamoja na kuwa mambo mengine yanasimamiwa na TAMISEMI lakini ninapokuwa katika ziara nikikutana na changamoto zinazowahusu nashughulikia kisha nawapa taarifa ili wachukue hatua stahiki, hivyo ndivyo tunavyoshirikiana katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Afya.”Alifafanua

Kuhusu upatikanaji wa dawa Dkt. Ulisubisya amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa tano upatikanaji wa dawa utakuwa umefikia asilimia 90% kutoka 70% za sasa na kuongeza kuwa suala la dawa limepewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo takribani shilingi 251 bilioni zimetengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.

No comments