Kifungo cha Maisha Jela Kwa Kumbaka Mama Mbele ya Mumewe na Watoto
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imewahukumu kutumikia kifungo cha maisha jela vijana wawili wakazi wa wilayani Chunya mkoani humo kutokana na kosa la ubakaji wa mwanamke mmoja waliyemtendea kitendo hicho mbele ya watoto wake.
Kadhalika, mahakama hiyo imewahukumu vijana hao wawili kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kutokana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo siku ya tukio walimjeruhi mume wa mwanamke waliyembaka.
Vijana waliokumbwa na vifungo hivyo viwili kutokana na mashitaka mawili yaliyokuwa yakiwakabili ni Ngaru Joseph (32) na Pili Mneme Kapigi (30) wote wakiwa ni wakazi wa wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Awali ilielezwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mazoya Luchagula, Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Alice Mkasela kuwa mnamo Julai 10, mwaka huu saa nane usiku nyumbani kwa mlalamikaji katika Kijiji cha Ukwavila wilayani Mbarali washitakiwa walivamia na kuvunja mlango nyumba ya mkazi huyo aliyekuwa amelala na mke na watoto wao.
Luchagula alisema walipofanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo washitakiwa hao walimjeruhi baba wa familia kwa kumkata na shoka kichwani kisha wakapora fedha kiasi cha Sh 580,000, wakachukua nguo zote za wanafamilia na kisha kumbaka mama wa familia mbele ya mumewe na watoto.
Mwendesha mashitaka huyo alisema wanafamilia hao kupitia mwanga wa taa ya sola waliweza kuwatambua watuhumiwa kabla wazazi hawajapelekwa Hospitali ya Misheni Chimala walikolazwa kwa ajili ya matibabu.
Kutokana na makosa hayo Luchagula aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine walio na tabia hizo wilayani hapa na kwingineko nchini.
Akito adhabu kwa washitakiwa, Hakimu Mkasela alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na pande zote mbili na kwamba kwa kosa la kwanza la unyangaji wa kutumia silaha washitakiwa watakapaswa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kwa kosa la pili la ubakaji watatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwao na watu wengine.
Awali washitakiwa waliiomba Mahakama kuwapunguzia adhabu wakisema bado umri wao ni mdogo na wanategemewa na familia zao, maombi ambayo yalitupiliwa mbali na hakimu Mkasela.
Post a Comment