Baba Achinja Wanawe Wawili na Kisha Kujinyonga
Watoto wawili wenye umri wa miaka mitatu na sita wa Kijiji cha Patane Kata ya Mambamiamba wilayani Same, wameuawa kwa kuchinjwa na panga na baba yao mzazi Yohana Greson (26) na yeye mwenyewe kujining’iniza kwenye paa la nyumba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 13, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi katika Kijiji cha Patane.
Kamanda alisema baba huyo alifanya tukio hilo la kutisha baada ya mkewe Eva Tumaini (29) mkazi Kijiji cha Ghona kwenda shambani na kumwacha mumewe nyumbani akiwa na watoto wawili, Esta Yohana na Tumaini Yohana, ambapo alichukua panga na kuwachinja na yeye kujinyonga kwa kamba.
Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba uchunguzi wa awali umebaini marehemu huyo alikuwa na tatizo la kifafa.
Alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba marehemu hakuacha ujumbe wowote na uchunguzi ukikamilika ndugu za marehemu watakabidhiwa miili hiyo kwa ajili mazishi.
Post a Comment