Kanali wa JWTZ aeleza sababu za kuteuliwa na CCM kuwa Katibu wa NEC , Siasa na Uhusiano wa Kimataifa
Kanali Ngemela Lubinga (katikati), kulia ni Msaidizi wa Kanali Lubinga, Meja Joseph Masanja na kushoto ni Kapteni Swaleh Omar.
****
Wakati watu mbalimbali wakiwa na maoni tofauti kuhusu Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Halmashauri Kuu yake kumteua Kanali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzaia (JWTZ) kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, mwenyewe ameibuka na kutolea ufafanuzi uteuzi huo.
Kanali Ngemela Eslom Lubinga amesema kuwa alishastaafu utumishi wake jeshini na kuwa angeweza kutumikia chama cha siasa kwani si mtumishi wa jeshi hilo tena. Kanali Lubinga aliyekuwa Msemaji wa JWTZ alisema kuwa alistaafu utumishi katika jeshi kuanzia Disemba 2 mwaka huu. Aidha, alisisitiza kuwa alijiunga na Chama cha Mapinduzi mwaka 1979.
Kikubwa kilichozua maswali kuhusu uteuzi huu ni kwa sababu wanajeshi na watumishi wengine wa umma hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya siasa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waraka wa Utumishi wa mwaka 2015 unakataza watumishi wa umma kuwa wanachama wa vyama vya siasa lakini unatambua haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Badhi ya maswali yaliyoulizwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii ni lini Kanali Lubinga alijiunga na CCM kiasi cha kuweza kuteuliwa katika nafasi ya juu kiasi hicho? Kama alijiunga na chama mwaka 1979 inaonyesha wazi kuwa alikiuka katiba ya nchi inayowataka wanajeshi kutojiunga na vyama vya siasa.
Akijibu swali hilo Kanali Lubinga alisema kuwa wakati wa mfumo wa chama kimoja wanajeshi waliruhusiwa kujiunga na chama cha siasa na kuwa baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ndipo walizuiwa na kadi walizokuwa nazo zilichukuliwa.
Kanali Lubinga aliendelea kusema kuwa kadi zile hazikutupwa bali zilihifadhiwa na hivyo baada ya kustaafu Disemba 2 mwaka huu akachukua kadi yake na kuendelea na uanachama wake.
Wengi waliokosoa uteuzi huo walitaka kuhakikisha kuwa siasa za nchi haziathiri utendaji wa majeshi yetu na utumishi wa watumishi wengine wa umma.
Post a Comment