Jaji Mutungi Atoa Usajili kwa Chama kipya cha CM-TANZANIA.
VYAMA vya Siasa nchini vimeaswa kuepukana na migogoro na kutumia vikao vyao katika kuendeleza shughuli zao za kisiasa.
Hayo yamesemwa leo na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mhe. Jaji Francis Mutungi wakati akikabidhi Cheti cha Usajili wa muda kwa Chama kipya cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA).
Aidha, Jaji Mutungi amevitaka Vyama vya siasa nchini kufanya siasa na sio uanaharakati kwaki kwa kufanya hivyo malengo yao yatatimia na kuifanya Tanzania kuwa na amani.
‘’Msipende kukimbilia kwenye vyombo vya habari mnapokuwa na migogoro bali malizeni tofauti zenu ndani ya vikao vyenu kulingana na Katiba ya Vyama vyenu’’, alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuwa, Tanzania inapaswa kuwa na vyama vya siasa vinavyojitambua na vinavyojua wajibu wao katika kuleta maendeleo ya Taifa kwani siasa sio chuki wala uasama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA) Bwana Laban Nkembo amesema kuwa, chama hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuiweka Tanzania kimaadili na uwajibikaji kwa kuwa kinabeba mambo makubwa mawili yakiwemo Amani na Upendo.
Ameongeza kuwa, chama chao sio cha Upinzani na kinaheshimu chama kilichopo madarakani hivyo, kinaahidi kushirikiana na Chama Tawala kuenzi mazuri yanayofanywa na chama hicho.
‘’Chama chetu sio cha upinzani, tunataka nchi nyingine duniani ziwe zinakuja kujifunza Tanzania kuhusu amani na maendeleo tulionayo’’, alisema Nkembo.
Aidha, amebainisha kuwa, chama chao cha CM-TANZANIA kitatoa ajira za kudumu kwa Wanachama wake na hata kwa wale wasiokuwa wanachama ambapo kimeshaandaa Idara ya usimamizi mzuri wa huduma kwa jamii kama vile Wazee, Wajane, Walemavu pamoja na Yatima.
CM-TANZANIA ni Chama cha 23 kupokea usajili baada ya Vyama vingine vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu.
Post a Comment