Header Ads

Magufuli apangua wakuu wa mikoa

                                                                                      RAIS John Magufuli
RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa huku akiwaacha wakuu wa mikoa 12 na kuwateua wapya 13. Katika uteuzi huo uliotangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mussa Iyombe, Rais Magufuli pia amewakumbuka mawaziri wanne wa zamani walioangushwa kwenye uchaguzi uliopita.
Aidha, amewapandisha wakuu wa wilaya watano, akiwemo Paul Makonda aliyekuwa Kinondoni ambaye sasa ataongoza Mkoa wa Dar es Salaam. Dk Magufuli amewabakiza wakuu wa mikoa saba katika vituo vyao vya kazi; watano wamehamishwa vituo vya kazi na mmoja amepangiwa mkoa mpya wa Songwe.
Kwenye safu hiyo ya wakuu wa mikoa, wamo wanajeshi wapya wanne. Pia wamo makada wawili maarufu wa CCM ambao ni Martine Shigela na Methew Mtigumwe. Wakuu hao wa mikoa wataapishwa kesho, Ikulu, Dar es Salaam.
Waliotemwa Wakuu wa Mikoa walioachwa na mikoa waliokuwa wakiiongoza kwenye mabano ni Ludovick Mwananzila (Tabora), Fatuma Mwassa (Geita), Issa Machibya (Kigoma), Mwantumu Mahiza (Tanga), Parseko Kone (Singida) na Abbas Kandoro (Mbeya).
Wengine ni Magalula Magalula (Rukwa) Rajabu Rutengwe (Morogoro), Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Asery Msangi (Mara), Elaston Mbwilo (Simiyu) na Ali Rufunga (Shinyanga). Ma-DC waliopanda Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda sasa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Pia Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Jordan Rugimbana ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Dodoma. Vile vile Antony Mataka aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, sasa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Zelothe Steven, amepandishwa na sasa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Zelothe amewahi kuwa Kamanda wa Polisi wa mikoa mbalimbali kabla ya kustaafu na kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Musoma Mjini. Wanajeshi walioula Wakuu wa Mikoa wapya walioteuliwa ni Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita na Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu anayekwenda Mkoa wa Kagera.
Wakuu wengine wapya wa mikoa ni Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma. Mawaziri wa zamani Aliyekuwa Naibu Waziri Kilimo, Ushirika na Chakula, Godfrey Zambi anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Zambi alishindwa ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliopita na mgombea wa Chadema, Pascal Haonga. Zambi pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya. Dk Steven Kebwe ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii katika serikali ya awamu ya nne, anakuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Alishindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita na mgombea ubunge wa Chadema, Marwa Ryoba. Aliyekuwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango pia ameteuliwa kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Kilango pia alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi tangu mwaka 2013 na aliangushwa kwenye ubunge na mgombea kutoka Chadema, Dk Naghenjwa Kaboyoka. Mwanasiasa mwingine aliyeanguka kwenye ubunge ni Aggrey Mwanri ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mwanri alikuwa Naibu Waziri wa Tamisemi katika serikali ya awamu ya nne. Aliangushwa ubunge na Dk Godwin Mollel wa Chadema. Makada wa CCM Martine Shigela ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Kabla ya uteuzi huo, Shigella alikuwa Ikulu akiwa mmoja wa washauri wa Rais katika masuala ya siasa. Kada mwingine ni Methew Mtigumwe ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Waliohamishwa vituo Kwa upande wa wakuu wa mikoa waliohamishwa vituo vya kazi ni Said Meck Sadick aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anayekuwa sasa Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.
Magesa Mulongo aliyekuwa Mwanza sasa anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa Mara, Amos Makalla aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro anakuwa wa Mkoa wa Mbeya. Wengine ni John Mongella ambaye amehamishwa kutoka Mkoa wa Kagera na sasa anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Chiku Galawa ambaye ametolewa Mkoa wa Dodoma kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Waliobaki vituoni Wakuu wa mikoa walioendelea kwenye vituo vyao vya kazi na mikoa husika kwenye mabano ni Daudi Ntibenda (Arusha), Amina Masenza (Iringa), Joel Bendera (Manyara), Halima Dendegu (Mtwara), Dk Rehema Nchimbi (Njombe), Evarist Ndikilo (Pwani) na Said Mwambungu (Ruvuma).
HABARI LEO

No comments