Aandaa maandamano kumpongeza Magufuli.
Dk Godfrey Malisa
ALIYEKUWA mgombea uspika wa Bunge la Tanzania, Dk Godfrey Malisa, amekusudia kuandaa maandamano ya kitaifa kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya kurejesha hadhi ya taifa ndani na nje ya nchi.
Maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika Aprili mwaka huu yatapokewa na wakuu wa mikoa nchini kote yakiwa na ujumbe wa kutaka watanzania kumuunga mkono rais katika kazi anazofanya ikiwemo kupambana na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na ukwepaji kodi.
Dk Malisa alitoa mfano wa wananchi walipounga mkono azimio la Arusha lililoasisiwa na Rais wa Awamu ya Kwanza Julius Nyerere kwamba walifanya hivyo bila kujali itikadi za dini, siasa na tofauti nyingine zozote bali walitanguliza mbele maslahi ya taifa.
“Kile kinachofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kinapaswa kuungwa mkono maana taifa limepata mkombozi anayefahamu matatizo ya watanzania...tumpe moyo aendeleze kazi nzuri anayofanya,”alisema.
Dk Malisa alisema maandamano hayo ambayo hayatakuwa na itikadi za dini au vyama vya siasa yatawashirikisha makundi yote ya kijamii wakiwamo wasomi, wafanyakazi, wafanyabiashara wa kada zote na wananchi wa kawaida lengo likiwa kutaka Watanzania kubadilika.
Alitaka wananchi kutojipendekeza kwa watoa huduma za aina mbalimbali katika ofisi za umma kwa kudhani kwamba bila kutoa rushwa hawatapata huduma stahili, badala yake wafuate sheria , kanuni na taratibu katika sekta husika ili kuondoa ushawishi wa kuombwa rushwa.
Aidha Dk Malisa alitaka wale wote wanaohitaji kuratibu maandamano katika mikoa yao kuwasiliana naye kwa namba 0716 810677, ili kushirikiana katika kufanikisha maandamano hayo na kuepuka kugeuzwa kuwa mtaji wa kisiasa.
CHANZO:HABARI LEO
Post a Comment