Header Ads

VIDEO: Mbowe Ajibu Malalamiko ya Viongozi wa NCCR-Mageuzi,chadema kujipa umiliki wa UKAWA.



MWENYEKITI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananachi (UKAWA), Freeman Mbowe amesema, wanaoleta chokochoko ndani ya umoja huo walitaka upendeleo.

Kauli ya Mbowe inakuja siku mbili baada ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Ghati Musore na katibu mkuu wa chama hicho Mosena Nyambabe kudai kwamba “Chadema imejipa umiliki wa UKAWA.”

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari viongozi hao wa NCCR-Mageuzi walimtuhumu mwenyekiti wao James Mbatia ‘kutekwa’ na Chadema na kwamba, ameshindwa kukitetea chama chao kwa kile walichosema kumezwa katika umoja huo.

Akizungumza na waandishi jana, Mbowe alisema viongozi hao wana jambo lingine nje ya yale waliyoyatamka hadharani na kwamba, kubwa ni kutaka kupewa upendeleo wa kugombea majimbo licha ya kukosa sifa.

“Tulikubaliana kuwa ili chama kipewe jimbo tutaangalia matokeo ya chama 2010, tutaangalia madiwani wa chama husika katika jimbo, mtandao wa chama pia matokeo ya uchaguzi wa vijiji na mitaa 2014 pamoja na mtandao wa ushindi wa mgombea” alisema Mbowe.

Mbowe alisema majimbo ambayo Nyambabe na Leticia wamekuwa wakiyang’ang’aniwa kugombea licha ya kutokuwa na sifa ni Segerea la jijini Dar es Salaam ambalo walipewa CUF na Jimbo la Serengeti lililopo Mara ambalo limekabidhiwa kwa Chadema.

“Nyambabe alihitaji kugombea Jimbo la Serengeti ambako Chadema ilishinda vijiji 38 lakini NCCR haikushinda hata kijiji kimoja katika uchaguzi wa vijiji, Chadema ina madiwani 8 NCCR haina hata mmoja, Nyambabe amegombea jimbo hilo mara mbili kwa vyama tofauti lakini hakupata hata asilimia 5, tungempaje hapo?” alihoji Mbowe.

Kwa upande wa Musore, Mbowe alieleza kwamba mwanamama huyo aliomba aachiwe kugombea katika Jimbo la Segerea ambako NCCR haina mtandao wa ushindi wala nguvu “jambo hili UKAWA tulilipinga.”

“Musore tunamfahamu aliwahi kuwa diwani wetu Tarime, hakujijenga wala kujenga NCCR, katika Jimbo la Segerea pia lakini akawa anataka tumzawadie jimbo kama makamu mwenyekiti taifa, hapana! tunataka kushinda hatuwezi kufanya uamuzi tunaojua wananchi wataukataa,”alisema Mbowe.

Hata hivyo alisema UKAWA bado wanaendelea na utatuzi wa migogoro iliyojitokeza katika majimbo na kwamba mambo yatakuwa mazuri muda si mrefu.

“Huu ni muungano wa vyama vinne, lazima kutofautiana kuwepo lakini kamwe hatuwezi kushindwa kuelewana katika maeneo machache yaliyobaki na hivi tunavyoongea Profesa Baregu, Salum Mwalimu, Bashage na viongozi wa CUF taifa wameelekea majimbo yenye shida,”alisema  Mbowe.

Baadhi ya majimbo yaliyo na utata ni Mtwara Mjini, Kigamboni, Itilima (Simiyu), Masasi, Mtama (Lindi), Ngara na Sikonge.

Msikilize Mbowe akiongea


No comments