WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameagiza mameneja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), watakaoshindwa kutekeleza maagizo ya wizara hiyo, waondolewe kazini ifikapo Machi mosi mwaka huu.
Alisema hayo wakati wa kikao chake na watendaji wa Tanesco na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofanyika katika kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni kuunganisha huduma kwa wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya ankara za umeme, kupunguza manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, ifikapo Machi mosi mwaka huu atatuthibitishia kama mameneja hawa wataendelea na majukumu haya wanayosimamia ama la, na hii itatokana na ufanisi wa utendaji katika majukumu tuliyowapangia,” alisema Profesa Muhongo.
Mbali na mameneja hao, Profesa Muhongo ameagiza Kitengo cha Uwekezaji cha Tanesco, kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo Aprili 2 mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo waondolewe katika nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni makubwa na tuna miradi mingi ya usambazaji umeme kwa wananchi ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa Umeme Vijijini).
“Wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi mipya ya umeme, tutashindwa kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha umeme tulichokuwa nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
Post a Comment