Saba Watiwa Mbaroni Mbeya Kwa Mauaji ya Mlinzi Wa SUMA-JKT
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia watu saba kwa matukio mbalimbali ya uhalifu, wakiwamo vijana watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mlinzi wa SUMA-JKT.
Wanadaiwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumpora bunduki na kutokomea nayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema Februari 26, mwaka huu ya saa 1:30 jioni, vijana hao wakiwa na mapanga, walimvamia na kumshambulia mlinzi huyo, Chewe Wilson (34), akilinda kituo cha mafuta cha Manyanya kilichopo Uyole.
Aliwataja vijana hao ni Hamis Shaban (19) na Ibrahim Mbilinyi (22) wote wakazi wa Itezi, Stan Wema (21) mkazi wa Uyole, Bahati Laulend (22) mkazi wa Iduda na Sambaa Samson (32) mkazi wa Isyeseye.
Alisema vijana hao baada ya kumjeruhi wakidhani amekufa walimpora bunduki aina ya Shortgun, mali ya SUMA-JKT aliyokuwa anaitumia na kutokomea nayo.
Hata hivyo, alisema mlinzi huyo alikutwa na wasamaria wema akiwa hai na kukimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya, lakini akafariki kesho yake kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata vijana hao na baada ya kupekuliwa walikutwa na bunduki hiyo waliyopora yenye namba za usajili 009009906-MP-18EM-M wakiwa wameificha nyumbani,” alisema Mpinga na kuongeza:
“Vilevile vijana hao wanaojiita ‘Doshaz’ walikutwa na mapanga matatu ambayo mojawapo lilitumika kumjeruhi Chewe na maganda matatu matupu ya risasi, tulipowahoji walikiri kuhusika na tukio hilo na tunatarajia kuwafikisha mahakamani upelelezi ukikamilika.”
Aliongeza kuwa vijana hao walieleza kuna mtu aliwatuma ili wakaibe bunduki hiyo kwa ahadi ya kupewa zawadi ya Sh. milioni tatu.
Katika tukio lingine, watu wawili akiwamo mzee wa miaka 60, wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la kutengeneza bunduki ya kienyeji aina ya Shortgun pamoja na kukutwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea silaha hiyo.
Mpinga aliwataja ni Mzee Fadhili Mayenga (60) na Mashaka Samuel (38), wote wakazi wa Kijiji cha Kambikatoto Wilaya ya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi Jumamosi mchana kufuatia msako mkali uliofanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Mpinga, baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengeneza silaha hiyo pamoja na risasi 25 za kienyeji ambazo hutumika kwenye silaha hiyo.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokuwa umekamilika.
Post a Comment