Gazeti Lapewa Onyo Kisa Picha za Mange Kimambi
Serikali imetoa onyo kwa gazeti la Tanzanite kwa kosa la kuchapisha picha za utupu.
Gazeti hilo la wiki, limechapisha picha ambazo ni kinyume cha maadili za mwanadada maarufu, Mange Kimambi.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema gazeti hilo ni miongoni mwa magazeti matatu yaliyopewa onyo kwa kipindi cha Mwezi Februari hadi mwanzoni mwa mwezi huu.
Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa upande wa redio, runinga na magazeti.
“Pale ambapo maadili ya uandishi yanakiukwa au changamoto za utekelezaji wa misingi, sisi hatutasita kuchukua hatua,” alisema.
Alibainisha magazeti hayo matatu likiwamo la Tanzanite yameonywa kwa kukiuka baadhi ya misingi ya uandishi wa habari.
“Moja ya magazeti yaliyoonywa ni pamoja na gazeti la Tanzanite, tumewaonya kwa sababu ni mara yao ya kwanza kuchapisha picha fulani za utupu, sio kuhusu ‘content’, ni kuhusu aina ya picha walizochapisha,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa kwa magazeti mbalimbali kwa nia njema ya kusisitiza weledi katika utendaji kazi kwenye tasnia ya habari.
Katika hatua nyingine, alisema katika kipindi cha Februari miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kimataifa ni ripoti ya hali ya rushwa na mapambano dhidi ya ufisadi duniani ambapo Tanzania imepanda katika mapambano hayo kwa nafasi 13 duniani.
Post a Comment