Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) adaiwa kutoweka Katika mazingira Ya Kutatanisha
Taarifa zilizoenea mchana huu zinadai kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hajulikani alipo tangu jana saa sita usiku.
Marafiki za Nondo wamedai alituma ujumbe kwa viongozi wenzake wa TSNP kuwa yuko katika hatari na baada ya kutuma ujumbe huo simu yake ilikuwa ikipokelewa lakini hakuwa akiongea chochote, na baada ya muda alianza kujiondoa kwenye magroup ya WhatsApp.
Taarifa kutoka kwa mmoja wa viongozi wa TSNP kuhusu Nondo inasema hajulikani alipo wakiwemo wazazi wake.
Viongozi wa TSNP wamefika Kituo cha Polisi kilichopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na kutoa taarifa za kupotea kwake.
February 18, 2018, Nondo alijitokeza na kuikosoa mienendo ya Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani, na mara ya mwisho kuongea na wanahabari, alishinikiza Waziri Mwigulu Nchemba ajiuzulu.
Akizungumza na wanahabari jana March 6 2018, Nondo aliwataka TAHLISO waache kuwa wasemaji wa wizara na serikali na kuwataka wakumbuke majukumu yao mazito ya kusemea wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu wanalipishwa ada vyuo vikuu.
“TAHLISO ambayo kila chuo kikuu nchini kinatoa ada isiyopungua shillingi laki tano kwa mwaka ili TAHLISO iweze kutetea maslahi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, imeacha kutimiza wajibu wake wa msingi na badala yake imegeuka kuwa taasisi yenye kusema kwa niaba ya serikali pamoja na kushambulia taasisi ambazo zinatetea maslahi ya wanafunzi nchini ikiwemo TSNP.
“Akwiline alikuwa ni mwanafunzi pia, TSNP ni mtandao wa kutetea wanafunzi, tunayo hayo mamlaka kusemea, kukemea, kushauri na hata kutoa mapendekezo yetu juu ya tukio lolote linaloashiria upotevu wa haki kwa wanafunzi. TAHLISO wanatoa wapi ujasiri, mamlaka ya kutuzuia TSNP tusitimize wajibu wetu?” alisema Nondo.
Post a Comment