Breki zilivyosababisha vifo 6 na majeruhi 6
WATU sita walifariki dunia jana na wengine sita kujeruhiwa baada ya lori la kokoto walilokuwa wakisafiria kufeli breki na kugongana na gari la taka la Manispaa ya Dodoma, katika gema la Mlima Ntyuka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba ilikuwa majira ya saa tisa alasiri.
Alisema ajali hiyo, imehusisha magari mawili ambapo moja ni lori la kokoto lenye namba T236 DHF na la taka la Manispaa.
Akizungumza kuhusu ajali hiyo, mmoja wa mashuhuda ambaye hakupenda jina lake liandikwe alisema lori hilo la kokoto lilipinduka katika mlima huo likiwa limebeba abiria ambao ni wapakia kokoto.
"Hili gari lilikuwa na abiria zaidi ya 10 ambao ni wapakiaji kokoto na lilikuwa likiendeshwa na Baraka Malata ambaye yupo mahututi kwa sasa," alisema shuhuda huyo. "Huyu Baraka huwa ni utingo wa hilo lori, dereva mwenyewe hakuwepo leo."
Alisema lori hilo lilikuwa likishuka na kokoto kutoka kwenye mlima huo na kwamba breki zake zilifeli na kugongana uso kwa uso na gari la taka ambalo lilikuwa likipandisha.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Dodoma, Dk. Caroline Damian alithibitisha kupokea miili sita ya watu waliofariki na kwamba baadhi ya majeruhi wapo katika hospitali hiyo na wengine Hospitali ya DCMC.
Post a Comment