Hospitali ya rufaa Mkoani Geita inayojengwa Mtaa wa Magogo kata ya Bombambili mjini Geita inatarajiwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya elfu moja wa nje na zaidi ya 480 watakaokuwa wakilazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Mwenyekiti wa bodi teule ya hospitali hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa majengo mkoani Geita Mhandisi Glads Jefta alisema katika hatua ya kwanza ya ujenzi wanaendelea na ujenzi wa majengo manne na wanatarajia kukamilisha baada ya miezi 9 ambapo umefikia asilimia 35.
“Tunatarajia hospitali hii itakapokamilika itahudumia idadi ya wagonjwa wa nje zaidia ya elfu moja na wa kulazwa mia nne na themanini na tunaamini ndani ya muda wa miezi mitatu ambayo tumeomba kuongezewa tutakuwa tumekamilisha ujenzI”Alisema Mhandisi Glads.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali Teule ya mkoa wa Geita Bw ,Simon Rweyemamu alisema walitarajia Hospitali hiyo ingekamilika ndani ya miezi 9 lakini kukosekana kwa umeme na maji ndio sababu zilizokwamisha mradi huo kwa kuwa Mkandarasi amekuwa akinunua maji kutoka nje na wakati mwingine kutumia mafuta kwa ajili ya jenereta.
Kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Geita Dr Joseph Odero alisema hospitali ya rufaa ya sasa ambayo ilikuwa ya wilaya ni ndogo kwa kuwa ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 150 hadi 200 na wale wa kulazwa 200 hadi 250 na kwamba hali ya wagonjwa kwa sasa ni kuanzia 300 hadi 350 hivyo kukamilika kwa hospitali hiyo ya rufaa kutasaidia kukabiliana na changamoto ya wingi wa wagonjwa
Mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa kwa sasa umefikia asilimia 35 kwa hatua ya kwanza ambayo inatarajia kugharimu kiasi cha Sh Bilioni 5.9
Post a Comment