Waziri Kigwangalla atolea ufafanuzi tuhuma za Mange Kimambi
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amefunguka na kujibu hoja ambayo Mwanaharakati wa mambo ya siasa mtandaoni, Mange aliibua kwenye mtandao wake Instagram kudai Waziri huyo ameshiriki kuwaingiza chaka Watanzania ili watapeliwe pesa
Waziri Kigwangalla akijibu hoja hiyo amesema kwamba yeye alialikwa kama mgeni wa heshima na kuwa alikuwa hawatambui watu hao binafsi na wala biashara yao alikuwa haitambui na alipoitwa kuzindua tawi lao hapa nchini alishindwa kuwakatalia ila hana maslahi binafsi katika kampuni hiyo.
"Nimeona nitoe ufafanuzi kwenye hili jambo. Maana kila mjadala juu ya hii kampuni ya ..... unapoibuka, jina langu linakuja, na mara nyingine picha yangu inawekwa. Ukweli ni kwamba, nilialikwa kwenye shughuli ya uzinduzi wake kama mgeni wa heshima; mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa wakati huo, Dr. Adelhelm Meru.
"Niliamini kwa heshima ya kuzinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ambao ndiyo wenye dhamana ya usajili wa biashara zote nchini, ni lazima ni watu halali na bado ninaamini kama kuna shida mamlaka husika zitachunguza na kuchukua hatua stahiki na kama hakuna shida basi ni vema mamlaka husika zikatoa mwongozo utakaowaondoa hofu wananchi wenzetu wenye ‘interest’ ya kushiriki kwenye biashara hii.
"Baada ya kufika eneo la tukio, kiitifaki ikaonekana nami lazima nishiriki zoezi, nikashindwa kukataa. Nadhani inafahamika kwamba nimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono kwa vitendo jitihada nyingi mbalimbali za wajasiriamali vijana ambao wameamua kutoka #NjeYaBox.
"Hata hawa nilishindwa kuwakatalia. Ukweli ni kuwa, siwajui wao binafsi ‘at personal’ level na wala biashara yao, umiliki wake na muundo wake siujui zaidi ya kuelewa kwa juu juu kuwa ni ‘network marketing’.
"Ifahamike hapa kuwa sina maslahi yoyote yale kwenye biashara hii na wala sikushiriki uzinduzi wake kwa malengo ya kutoa ushawishi ili watu wajiunge, na natoa rai kwamba wanaotaka kujiunga ama kuacha kujiunga wasitumie picha za ushiriki wangu siku ya uzinduzi, kwa namna yoyote ile, kujenga uhalali wa aina yoyote ile, bali watumie vipimo vyao vingine kufanya uamuzi na siyo picha zangu" alisema Kigwangalla
Mbali na hilo Waziri Kigwangalla aliwaonya watu mbalimbali na Taasisi ambazo zimekuwa zikitumia picha yake hiyo kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika biashara hiyo na kusema hatahusika na matokeo yoyote yale na kuwa akibaini kuna mtu au Taasisi inafanya hivyo atachukua hatua za kisheria.
"Sintohusika na matokeo yoyote yale, chanya ama hasi, ya ushiriki wa mtu yeyote yule ama taasisi yoyote ile, kwenye shughuli za kampuni hii.
"Naomba pia izingatiwe kwamba, jina langu ama picha yangu haijaruhusiwa kutumika kama bango la matangazo ya biashara ya mtu au taasisi yoyote ile, na hivyo kufanya hivyo ni kosa kisheria na ikibainika nitachukua hatua kali za kisheria" alisisitiza
Post a Comment