Ndugu Wasimulia Jinsi Viongozi Wawili Walivyouawa KIBITI Huku Mmoja Akitobolewa Macho Yote
Risasi tano zimetumika kuwaua Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, kisha kumjeruhi machoni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Waliofariki katika tukio hilo ni Ofisa Mtendaji, Mwarami Shamte aliyekutwa na majereha matatu ya risasi na Mwenyekiti wa Kijiji, Hamis Bakari Mkima aliyekutwa na jeraha moja.
Pia wauaji hao walimpiga, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo, Michael Martin risasi ya macho, iliyoharibu macho yake mawili.
Kama hiyo haikutosha, waliichoma moto nyumba ya Martin na kisha kutokomea kusikojulikana.
Mganga wa zamu katika Kituo cha Afya Kibiti, Dk Sadock Bandiko alithibitisha kuuwawa kwa viongozi hao wa kijiji hicho.
Amesema Shamte amekutwa na majeraha matatu yaliyotokana na kupigwa risasi.
“Shamte alipigwa risasi moja kichwani na risasi mbili tumboni,”amesema.
Kwa upande wa mwenyekiti wa kijiji hicho, Dk Sadock amesema marehemu alipigwa risasi moja ya shingoni aliyopigwa toka upande wa kulia na kwenda kushoto lakini haikutokeza.
Pia alisema mwenyekiti huyo alikuwa na jeraha kubwa katika mguu wake wa kushoto lililotokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Mganga Mkuu wa Hospital ya Mchukwi, Dk Zacharia Lukeba alipolazwa Martin, amesema alipigwa risasi moja ya kichwani iliyofumua na kuharibu kabisa macho yake.
Amesema tayari wamempa rufaa kwenda Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Mmoja wa ndugu za marehemu hao amesema watu wanne waliokuwa na bunduki wakiwa wamevaa nguo nyekundu na kuficha sura zao kwa soksi walivamia kijijini hapo saa nne usiku wa kuamkia jana.
Amesema watu hao walianza kwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho (Hamis Bakari Mkima) (30) ambaye alifanikiwa kuwakimbia kabla hawajamfikia.
Amesema watu hao walimpiga na kitu chenye ncha kali katika mguu wake wa kushoto kisha kumrejesha kwake huku wakimtaka awapeleke kwa viongozi mbalimbali wa kijiji hicho.
Alieleza kuwa baada ya hapo walimtaka awapeleke kwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho (Mwarami Shamte) (40) na baada ya kufika huko walimpiga risasi tatu na alifariki dunia papo hapo.
Amesema watu hao bado walimtaka mwenyekiti huyo awapeleke kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo na baada ya kufika kwake walimpiga risasi ya usoni iliyoharibu macho yake.
Amesema baada ya hapo walimpiga risasi moja mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Mangwi, (Hamis Mkima) na alifariki papo hapo.
Pia ameeleza kuwa wakati watu hao wakifanya hayo walikuwa tayari wamechoma moto nyumba ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo kwa kutumia mafuta ya petroli yaliyokuwemo kwenye pikipiki yake na kuteketeza kabisa nyumba yake yote.
Mdogo wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo (aliyepofuliwa macho) aliyejitambulisha kwa jina la Paul Martin amesema tukio hilo limetokea usiku wa jana saa 4 ikiwa ni muda mfupi tangu aagane na kaka yake.
“Nilikuwa nyumbani kwake na nimeondoka wakati huo huo kwenda kulala baada ya dakika chache kupita, tulianza kusikia kelele za watu nisiowafahamu wakiwa kwenye nyumba ya kaka yangu,” amesema.
Paul amesema baada ya kusikia kelele hizo alitoka nje ili ashuhudie lakini kabla hajafanya lolote aliwekwa chini ya ulinzi kwa kumulikwa tochi na kutishiwa kupigwa risasi.
"Niliona watu kama watano wakiwa na silaha ambao waliniweka chini ya ulinzi baada ya kunimulika tochi," alisema.
Amesema baadhi ya watu hao walikuwa ndani ya nyumba ya kaka yake wakiendelea kumhoji huku wakiwa wamefunika sura zao.
Ameongeza kuwa baada ya hapo watu hao waliondoka na kaka yake kwenda kusikojulikana na baada ya muda mfupi walirudi naye.
Amesema watu hao baada ya kurejea naye waliwaamrisha watoto wake waliokuwa wamelala kutolewa nje kisha walichukua mafuta ya petroli yaliyokuwa kwenye pikipiki ya kaka yake kisha kuyamwaga ovyo kwenye nyumba hiyo na kuichoma moto.
Amesema baada ya tukio hilo waliondoka naye kwa mara ya pili na kwenda naye kusikojulikana kisha wakampiga risasi ambayo imeharibu macho yake yote.
Amesema baada ya kumpiga risasi hiyo walimtelekeza katika barabara iendayo katika kijiji cha Misimbo ambapo walimkuta jana asubuhi akiwa hajitambui.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.
Post a Comment