BABA AlLIUZA KUNI NA KUNISOMESHA HADI CHUO KIKUU
Ukitafuta jina la baba yangu (Joseph Kimanzi) kwenye mtandao wa Google, hutopata jibu lolote. Hakuna kitabu wala makala inayomhusu lakini kwetu sisi, yeye ni shujaa. Namuombea dua kwa Mungu kwakuwa alijitolea kila kitu kwa ajili yetu hivyo apate maisha marefu na aje kupumzika na kufurahia matunda ya kazi kubwa aliyoifanya kwa ajili yetu.
HAJAWAHI KUAJIRIWA SEHEMU YOYOTE
Kwa kadri ya kumbukumbu zangu zinavyoniambia, hajawahi kupata ajira ya kudumu ila alikuwa anafanya kila kibarua kitakachojitokeza mbele yake, mradi apate kitu cha kuleta nyumbani jioni atakaporudi. Tulikuwa tunaishi karibu na mjini, kwahiyo hatukuwa na shamba kusema tutalima. Baba alikuwa anafanya kazi kwenye majumba ya watu na kuuza kuni, mkaa na chochote atachoona kitampatia pesa.
Hakuwa anachagua kazi ya kufanya. Hata angetaka kuchagua, hakuwa na cha kuchagua vile vile. Kwahiyo ilimlazimu kufanya kilicho mbele yake.
Hakuwahi kupata anasa ya kulala zaidi ya alfajiri. Hakuna hata siku moja niliyoamka na kumkuta baba nyumbani, sio tu kitandani. Alfajiri ilikuwa ikimkuta akiwa maili kadhaa kutoka nyumbani. Asubuhi zote zilikuwa zinamkuta akiwa kwenye mapori akitafuta kuni nzuri kwa kuuza au kuchoma mkaa, au angekuwa njiani kwenda kutafuta maji, hitaji adimu sana kwenye eneo letu katika kipindi hicho, au angekuwa anafanya kazi za ujenzi. Mara kadhaa alirudi na majeraha yaliyotokana na panga lake kukosa mti anaokata na kutua kwenye kidole, au matofali yakimdondokea alipokuwa kwenye ujenzi – lakini hiyo haikutosha kumfanya achelewe kuamka wala kutokwenda kibaruani kabisa; aliamka na kwenda kutafuta pesa tuweze kuishi.
HAKUWAHI KULALAMIKA
Jambo la kushangaza sana ni kwamba hakuwahi kulalamika, hata alipokuwa anaumia, hata alipokuwa amechoka sana na kuwa na maumivu ya mifupa. Mara zote alikuwa akituangalia na kutabasamu na kutuasa tusome kwa bidii sana. Tabu alizokuwa anazipitia kwa ajili yetu zilinifanya niamue kusoma kwa juhudi sana. Mara zote alikuwa akiniambia kuwa Mungu ametubariki kwa kutupa afya njema na akili, tunachotakiwa kufanya ni kuvitumia, na nilimuamini.
IMANI YAKE ILINIPA MATUMAINI
Nilifanya mtihani wa kuhitimu Shule ya Msingi wakati watu walionizunguka walikuwa na uhakika kuwa baba asingeweza kunisomesha sekondari, na hawakusita kuniambia hivyo wazi wazi. Nilikata tamaa, lakini wiki chache kabla ya mtihani wa kuhitimu aliniambia:
“Usiwasikilize, usiangalie unapotoka, fanya jitihada zako zote na nitakupeleka shule ya sekondari.” Na alitimiza ahadi yake.
Nilikuwa wa pili darasani kwangu na nilikuwa wa kwanza kwa watahiniwa wa kike kwenye matokeo. Nilikuwa najua kwamba hakuwa na pesa ya kunilipia ada, lakini alichokisema kilinipa matumaini makubwa.
Ingawa nilikuwa wa mwisho kuwasili shule na sikwenda shule ya chaguo langu, lakini nilikwenda shule. Baba aliweza kukusanya robo ya ada iliyotakiwa na kuniandikisha shule. Sijui aliwezaje kumshawishi mkuu wa shule kunipokea lakini nakumbuka furaha niliyokuwa nayo!
ALIFANYA KAZI SHULE KWANGU KULIPA DENI
Ili kulipa kiasi cha pesa kilichobaki, baba alilazimika kufanya kazi shuleni kwangu, mara nyingi kwa kupeleka kuni. Nakumbuka alipokuwa akikodi lori, kulijaza kuni na kulileta shuleni. Walipofika shuleni, wenye gari walimwaga kuni hizo bila kuzipanga na kumwacha baba akifanya kazi hiyo peke yake. Mara nyengine wakati wa mapumziko nilikuwa nikipita karibu na kuni hizo na kujikuta nikishangaa imewezekanaje mtu mmoja kukata kuni zote hizo, achilia mbali kuzipanga. Nilipomsogelea kumsalimia mara zote alitabasamu lakini hakuweza kuficha uchovu na usingizi aliokuwa nao.
Lakini aliendelea kufanya kazi tu. mwisho alirudi nyumbani akiwa taabani kabisa, akiwa na njaa na majeraha mikononi na miguuni. Kibaya zaidi ni kwamba shule haikumpa hata senti moja, hata nauli tu ya kumuwezesha arudi nyumbani. Pesa yote aliyotakiwa kulipwa iliingizwa kwenye ada yangu. Alirudi nyumbani bila chochote mfukoni, lakini alifurahi kwamba nitabaki shule. Nilitamani kumsaidia. Mara nyingine nilijikuta nalia nikiwa peke yangu kwa kumhurumia.
Alikuwa na imani na mimi na alitamani siku moja niende nje ya nchi kujiendeleza kimasomo.
IMANI YAKE KWANGU, KWA MARA NYINGINE
Imani yake kwangu, kwa mara nyingine tena, ilinifanya niamue kusoma kwa bidii kubwa sana na kushika nafasi ya kwanza katika Wilaya yangu kwenye mtihani wa kuhitimu sekondari. Ingawa sijaenda kusoma nje ya nchi kaka baba alivyotamani lakini nilipata nafasi ya kusoma Chuo Kikuu nchini.
Leo hii mimi ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta, nina shahada ya Ununuzi na Ugavi na wadogo zangu wawili wapo sekondari, shukrani za kipekee kwa baba. Yeye ni shujaa wangu na namfurahia kila uchao.
Post a Comment