Makonda ‘kizimbani’ Kamati ya Bunge.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imemhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa saa tatu kuhusu tuhuma za kuingilia madaraka ya mhimili huo wa dola na imesema imemaliza kazi na taarifa yake itaiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Makonda alifika mjini hapa, ikiwa ni hatua ya kuitikia mwito wa kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa na Bunge, Februari 8, mwaka huu katika kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge kwamba mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam ahojiwe na Bunge.
Katika kikao hicho, Bunge liliazimia kwamba Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti waitwe mbele ya Kamati hiyo ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma zinazowakabili dhidi ya mhimili huo.
Akizungumza baada ya kamati hiyo kumaliza kazi yake, Mwenyekiti wake, George Mkuchika alisema imekutana jana baada ya kuagizwa na Spika wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Tumefanya kikao hiki cha Kamati baada ya kuagizwa na Mheshimiwa Spika kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni zetu, Kamati hii inakutana pale tu inapoagizwa na Spika wa Bunge. Napenda kutoa taarifa kwamba Mheshimiwa Makonda leo (jana) amekuja mbele ya Kamati na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na Kamati imemaliza kazi yake,” alisema Mkuchika ambaye ni Mbunge wa Newala (CCM).
Mwenyekiti huyo alisema hatua inayofuata kama ilivyo utaratibu, Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa Spika kwa mujibu wa Kanuni, na Spika ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu kazi ya kamati hiyo.
Mkuchika alisema Spika aliiagiza kamati hiyo imuite Makonda mbele ya kamati kutokana na azimio hilo la Bunge lililopitishwa Februari 8, ambapo pamoja na mambo mengine mkuu huyo wa mkoa alitakiwa kufika mbele ya kamati kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Alisema kwa mujibu wa Azimio hilo, Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.
Anatuhumiwa kuingilia haki, uhuru na madaraka ya Bunge. Makonda aliwasili bungeni Dodoma saa nne asubuhi.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu lini Mkuu wa Wilaya ya Arumeru atahojiwa na kamati, Mkuchika alisema kamati yao inafanya kazi kwa agizo la Spika hivyo wanasubiri agizo hilo, watamuita kuhojiwa kama walivyofanya kwa Makonda.
“Sisi tunafanya kazi chini ya Spika, hatuiti mtu, tunatekeleza matakwa ya Bunge kupitia agizo la Spika,” alieleza Mkuchika alipozungumza na gazeti hili jana.
Post a Comment