WALIMU MKOANI GAEITA KUADHIBIWA KWA VINYAGO
Serikali mkoani Geita imeagiza halmashauri kuchonga vinyago na kuviweka kwenye meza za wakuu wa shule ambao shule zao zimefanya vibaya kwenye mitihani ya taifa ya darasa la saba ili kila atakayeingia ofisini akione.
Pia, zimetakiwa kuandaa vyeti kwa kila mwalimu ambaye wanafunzi wamefeli somo lake na kukiweka eneo analokaa kikiwa na maandishi yenye kuonyesha kuwa somo lake limefanya vibaya.
Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Rehema Mbwilo alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha kutangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kilichohudhuriwa na wadau wa elimu.
Alisema wanafunzi 26,376 walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, waliofanya ni 26,164, huku waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni 22,742 sawa na asilimia 86.92. “Mwalimu huyu pamoja na cheti cha kufanya vibaya kuwekwa eneo analokaa, pia lazima atoe sababu za somo lake kufanya vibaya. Lengo ni kuhakikisha shule za Serikali nazo zinafanya vizuri na hili litakuwa likifanywa kila mwaka,” alisema.
Alisema Geita ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri kwenye mtihani huo kwa kupata asilimia 86.92 na kushika nafasi ya kwanza kitaifa, lakini bado shule za Serikali zimefanya vibaya.
Katibu tawala wa mkoa aliyekuwa mwenyekiti wa kikao, Celestine Gesimba alisema usimamizi mbovu wa shule ni moja ya sababu zinazofanya shule za Serikali kufanya vibaya.
“Mkuu wa shule akishapewa cheo anajisahau, hasimamii tena walimu wala wanafunzi. Kwanza, yeye anajitoa kwenye vipindi hafundishi, nendeni kwenye shule binafsi muone usimamizi ulivyo,” alisema Gesimba.
Mkuu wa Wilaya ya Chato ambaye pia ni kaimu mkuu wa Wilaya ya Geita, Shaban Ntarambe aliwataka walimu wasiogope kuwachapa wanafunzi watukutu na wasio waoga viboko vilivyohalalishwa.
Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko alisema shule za Serikali zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo wingi wa wanafunzi na ukosefu wa chakula cha mchana.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
Post a Comment