Header Ads

Mwanzilishi wa Jamii Forums Jana Hakufikishwa Mahakamani.......Polisi Walivamia Ofisi zake na Kufanya Upekuzi

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam  limevamia ofisi za mtandao wa Jamii Forums (JF) na kufanya upekuzi na  kuondoka  na  nyaraka za usajili wa Jamii Media ikiwemo cheti cha mlipa kodi, cheti cha BRELA, leseni ya biashara, n.k..

Askari hao walivamia ofisi hizo jana mchana wakiwa wamefuatana  na  na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao  huo, Maxence Melo, wakafanya  upekuzi na kuwahoji baadhi ya wafanyakazi.

Baada ya kufanya upekuzi ndani ya ofisi hiyo walielekea nyumbani kwa mkurugenzi huyo,  kufanya upekuzi kabla ya kumrudisha  rumande kwa vile hakufikishwa mahakamani.

Melo alikamatwa  juzi  na   kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi  ambako aliwekwa selo.

Anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia upelelezi wa makosa ya mtandao kwa kushindwa kutoa taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums ambazo polisi walizihitaji.

Taarifa iliyotolewa jana na mtandao huo iliwataka watumiaji wake kutokuwa na hofu yoyote na kwamba Jamii Forums haina server Tanzania wala Africa .

"Tunaomba umma utambue kwamba Jamii Media haina servers wala min-server ofisini kwake, nchini Tanzania wala Afrika. Pili, tunaomba watumiaji wa JamiiForums.com wasitiwe wasiwasi juu ya usalama wa taarifa zao. 

"Teknolojia tunayoitumia (encryption) kumsajili mtumiaji wa JamiiForums.com haituwezeshi kumfahamu mtumiaji yeyote labda yeye akubali kwa hiari yake kujiweka wazi mtandaoni." Ilieleza taarifa hiyo

No comments