Mbunge wa Budalang’i nchini Kenya Asimulia Jinsi Rais Magufuli alivyoiteka Kenya
Mbunge wa Budalang’i nchini Kenya, Ababu Namwamba amesema Rais John Magufuli anavuma kwa umashuhuri nchini humo akitajwa kwa namna anavyopambana na ufisadi na kubana matumizi ya Serikali, lakini akasema sifa hizo zitapendeza iwapo huduma muhimu kwa wananchi zitaboreshwa na kuthibitika kwenye tafiti zitakazofanywa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati alipohudhuria mkutano wa demokrasia ulioandaliwa na ACT – Wazalendo jana, Namwamba ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Labour of Kenya (LPK), alisema Rais Magufuli ana mtandao Kenya unaomshabikia kwa uongozi wake, ikiwamo harakati zake za kupambana na ufisadi
“Lakini swali kuu katika fikra za Wakenya wengi ni sasa je, mambo yote tunayoona kwenye vyombo vya habari ni porojo tu ama ile inaitwa propaganda au ni masuala kweli yanayobadili maisha ya Watanzania wengi? Hivyo ingawa sifa za Magufuli zinaenea huku na kule, tungependa kuona mabadiliko halisi hapa Tanzania,” alisema.
“Tungependa kuona kwa mfano takwimu za ufisadi zimepungua. Takwimu za kuonyesha hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida imebadilika huduma kama vile maji, elimu na afya kwamba kweli zimebadilika hilo ndilo la muhimu zaidi, kinyume cha hapo hatutapata sababu ya kuamini au kuona kwamba mabadiliko hayo ni halisi.”
Namwamba, ambaye Julai 7 mwaka huu alijiuzulu ukatibu mkuu wa chama cha ODM kinachoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Raila Odinga baada ya kutoelewana, alisema siasa za nchi hizo mbili zinakaribiana kwa kuwa mashindano ya wanasiasa yaliyopo nchini ni kama yalivyo Kenya.
“Kila mara mnapokuwa na uchaguzi hapa sisi hutazama kwa makini sana kwa sababu kuna mengi ya kujifunza.
"
Hata hivyo, Namwamba alionya kuwa suala la ukabila nchini ni la kutiliwa maanani kwa kuwa kufanya siasa kwa misingi hiyo kumesababisha maafa makubwa ikiwamo mgawanyiko kwa wananchi.
Alisema siasa nzuri zinazopaswa kuendelezwa nchini ni zile za kuwaleta wananchi pamoja na kama ni mashindano, yawe ya sera, dhana, huduma bora kuliko kumtazama kiongozi wa chama au mgombea kwa kabila lake.
Alisema amekuja nchini kushirikiana na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe kupanda mbegu ya ushirikiano na kwamba atashiriki kuhamasisha vijana kutambua viongozi walioweka historia wakiwamo Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela.
Zitto akizungumza katika mkutano huo alieleza kuwa chama chake kinaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kurejesha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma na kupambana na ufisadi.
“Lakini tungependa kuona hatua zinachukuliwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vinavyohusika watumishi 154 wachukuliwe hatua zinazostahili.Pia suala la Escrow nalo linapaswa kuchukuliwa hatua na mengine mengi.”
Mshauri wa ACT, Profesa Kitila Mkumbo aliwasilisha mada ya; “Sisi ni kina nani?” akilenga kuwaelimisha wanachama wake kujihusisha na maisha ya watu, kwa kuwa kushughulikia changamoto na matatizo ni mchakato unaoendelea iwe ndani au nje ya Serikali.
“Chama chetu siyo cha kuvizia makosa ya Serikali ndipo tufanye siasa, tunajipanga kushindanisha ubora wa sera, kina itikadi yake kamili, ni jukumu letu kukosoa Serikali lakini jambo la muhimu ni kuonyesha tuna vitu gani bora kwa wananchi.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye alitoa mada iliyohusu masuala ya Katiba alisema mchakato wa Katiba hauna budi kurudishwa nyuma kwa hatua moja hadi kwenye rasimu.
“Kuna mambo mengi yamejitokeza ambayo yamewachanganya wananchi, hivi sasa wengi wanatofautiana hawajui uliishia kwenye hatua gani. Pia, hali iliyojitokeza kule Zanzibar ambapo wakati unajadiliwa awali kulikuwa na Serikali ya umoja ambayo sasa haipo. Kuna mambo mengi ambayo tumekuwa tunarudi nyuma hatua tano kisha kwenda mbele hatua mbili.”
Post a Comment