Rais wa zamani wa Israel Shimon Peres afariki dunia
Waziri mkuu wa zamani wa Israel aliyewahi kuhudumu pia kama rais Shimon Peres amefariki dunia akiwa na miaka 93.
Aliugua kiharusi wiki mbili zilizopita na hali yake ikawa mbaya zaidi ghafla Jumanne.
Bw Peres, ambaye alikuwa mmoja wa waliosalia kutoka kwenye kizazi cha wanasiasa waliokuwepo wakati wa kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948, alihudumu kama waziri mkuu wa nchi hiyo mara mbili na mara moja kama rais.
Alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1994 kwa mchango wake katika mashauriano yaliyopelekea kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya Israel na Palestina mwaka mmoja awali.
Wakati mmoja, aliwahi kusema kwamba Wapalestina ndio "majirani wa karibu zaidi" wa Waisraeli na wanaweza kuwa "marafiki wa karibu zaidi".
Bw Peres amefariki akitibiwa katika hospitali moja iliyopo karibu na mji wa Tel Aviv mapema Jumatano, jamaa zake wa karibu wakiwa karibu naye.
Alikuwa amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Sheba Medical Centre baada ya kupatwa na kiharusi 13 Septemba.
Rais wa Marekani Barack Obama amemweleza Bw Peres kama "rafiki wa karibu" kwenye taarifa, na akasema: "Aliongozwa na maono ya heshima na utu na alifahamu kwamba watu wenye nia njema wanaweza kustawi pamoja."
Bw Peres alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa pamoja na Waziri Mkuu Yitzhak Rabin, ambaye baadaye aliuawa, na Kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat.
Shimon Peres alikuwa nani?
- Alizaliwa 1923 Wisniew, Poland, eneo ambalo sasa hufahamika kama Vishneva, Belarus
- Alichaguliwa kwenye Knesset (Bunge la Israel) mara ya kwanza mwaka 1959
- Alihudumu katika serikali 12, mara moja kama rais na mara mbili kama waziri mkuu.
- Alitazamwa kama mpenda vita miaka yake ya awali - aliongoza mashauriano ya kuitafutia silaha Israel ilipokuwa bado taifa changa
- Alikuwa kwenye serikali iliyoidhinisha sera ya kujengwa kwa makazi ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalestina yaliyotekwa na Israel
- Hata hivyo, alitekeleza mchango muhimu katika kupatikana kwa Mkataba wa Amani wa Oslo, mkataba wa kwanza kati ya Israel na Wapalestina, uliosema wangefanya juhudi "kuishi kwa amani pamoja".
Mwanzoni mwa maisha yake kisiasa, alipewa jukumu la kusimamia wanajeshi na ununuzi wa silaha za kutumiwa na Haganah, jeshi la Israel.
Aliingia kwenye mkataba na Ufaransa wa kuipa Israel ndege za kivita aina ya Mirage. Aidha, alisaidia kuanzisha kiwanda cha siri cha nyuklia cha Israel.
Alikuwa waziri wa ulinzi mwaka 1976, watekaji nyara kutoka Palestina walipoteka ndege ya Israel na kuielekeza hadi Entebbe, Uganda. Aliongoza juhudi za kuwaokoa zaidi ya mateka 100.
Zamani alitetea makao ya walowezi wa Kiyahudi Ukindo wa Magharibi lakini baadaye akageuka mtetezi mkuu wa amani. Mara nyingi, alizungumzia haja ya kutokuwa na msimamo mgumu kuhusu maeneo ya ardhi ya Wapalestina.
Aliendelea kutekeleza shughuli nyingi za umma uzeeni, kupitia shirika lake lisilo la kiserikali la Peres Centre for Peace, ambalo hutetea uhusiano wa karibu baina ya Waisrael na Wapalestina.
Mwaka 2013 alisema: "Hakuna mbadala wa amani. Hakuna maana ya kwenda vitani."
Alistaafu kutoka wadhifa wake kama rais mwaka 2014.
CHANZO:BBC
Post a Comment