Header Ads

Serikali Ya Tanzania Yasema Haitajitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).


SERIKALI imesema Tanzania haitajitoa katika Mahakama ya Kimataifa yaMakosa ya Jinai (ICC). Hata hivyo, imesema tabia ya ubaguzi dhidi ya viongozi wa Bara la Afrika inayooneshwa na mahakama hiyo inaweza kurekebishwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Agustine Mahiga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Siku 100 za Rais John Magufuli tangu aingie madarakani.

“Sisi ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini mkataba wa Roma ambao ulianzisha Mahakama ya ICC… Tunataka kuona baadhi ya mambo yakirekebishwa ili kuondoa kile kinachoonekana kuwa ni ubaguzi kwa viongozi wa Afrika,” alisema Balozi Mahiga.

Waziri huyo alisema, katika Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano Tanzania imeweza kufanikiwa katika mambo mengi kupitia Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya uhusiano na migogoro mbalimbali.

Alisema tangu alipoapishwa kuwa Waziri ameshughulikia baadhi ya migogoro ukiwemo wa Burundi ambapo Rais Magufuli alimuagiza kwenda nchini humo ili kuzungumza na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza ili akubali kufanya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa mgogoro unaoendelea nchini mwake.

Balozi Mahiga alisema, hatua ya Rais kuzuia safari za nje kwa watumishi imesaidia kupunguza gharama ambazo wakati mwingine zilikuwa si za lazima, hivyo ni jambo ambalo linapaswa kupongezwa.

“Si kwamba Rais hatasafiri, hapana ila kwa sasa tunajua bado ana jukumu kubwa la kujenga serikali yake. Serikali si kwa maana ya Mawaziri tu ila watendaji wote kwa ujumla. Mambo yakishatulia nadhani hata yeye sasa ataweza kusafiri kwa safari atakazohitajika,” alisema.

No comments