Header Ads

MCHUNGAJI ADAIWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI YATIMA.

MCHUNGAJI Vitusi Yustus wa Kanisa la TAG lililopo Mwasele B, Manispaa ya Shinyanga, anadaiwa kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha kwanza ambaye ni yatima.
Hayo yalisemwa jana na mlezi wa binti huyo, Shija Lugendo, wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake.
Lugendo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mchungaji huyo alimrubuni mwanafunzi huyo ajiunge na kanisa hilo ili awe anamuombea.
Alidai mwanafunzi huyo alikubali kujiunga na kanisa hilo na sasa ana ujauzito unaoelezwa kuwa ni wa mchungaji Yustus.
Kwa mujibu wa mlezi huyo, baada ya kugundua kuwa ana ujauzito, mwanafunzi huyo aliaga shuleni kwa kueleza kuwa anaumwa.
“Huku nyumbani nako aliogopa kufika na kuamua kwenda kwa ndugu zake wengine walioko katika eneo la Ng’wagosha,” Lugendo alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kuona harejei nyumbani, waliamua kumfuatilia na kumrudisha nyumbani ambapo, kutokana na hofu aliyokuwa nayo, aliamua kujieleza mwenyewe kwa kusema kuwa hawezi kwenda tena shuleni kwa sababu ni mjamzito.
Pia, mlezi huyo alisema kuwa mwanafunzi huyo alimtaja mchungaji huyo kuwa ndiye aliyempa ujauzito.
Binti huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mchungaji siku ya kwanza kukutana alimueleza amuombee na kujiunga na kanisa hilo na alianza kwa kumpatia fedha kiasi cha Sh 5,000 na kudai anampenda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne alisema tuhuma hizo hazijafika kwao ingawa waandishi wa habari walimueleza kuwa tayari wanaomtuhumu mchungaji huyo wamepatiwa RB yenye kumbukumbu namba Shy/7830/2016.

No comments