Katibu Tawala, Mkurugenzi mbaroni fedha za tetemeko
POLISI mkoani Kagera inamshikilia na kuanza uchunguzi wa awali dhidi ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa, Amantius Msole aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Kelvin Makonda na watu wengine wawili kwa tuhuma za kufungua akaunti bandia ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Augustine Ollomi amethibitisha kushikiliwa kwa watu hao wawili na Mhasibu wa Mkoa huo, Simbaufoo Swai huku Meneja wa tawi la CRDB mkoani Kagera, Carlos Sendwa akiunganishwa katika uchunguzi wa tuhuma hizo.
Amesema Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi zaidi ya watuhumiwa hao.
Kwa mujibu wa Kamanda Ollomi, uchunguzi wa suala hilo hautachukua muda mrefu kabla ya watuhumiwa hao kufunguliwa mashtaka.
Baadhi ya wananchi wameunga mkono hatua iliyochukuliwa na Rais John Magufuli ya kutengua nafasi ya Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Kagera na kusema itaimarisha uadilifu na uwajibikaji mahala pa kazi miongoni mwa watendaji.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo, kwa sababu liko kwenye vyombo vya kisheria.
Juzi Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Msole na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Makonda.
Mhasibu wa Mkoa, Simbaufoo Swai amesimamishwa kazi baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo "Kamati Maafa Kagera" kwa lengo la kujipatia fedha.
Post a Comment