Header Ads

MAKALA KUHUSU FALSAFA, DHANA NA UMUHIMU WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU
 




MAKALA KUHUSU FALSAFA, DHANA NA UMUHIMU WA    MBIO ZA MWENGE WA UHURU
Falsafa ya Mwenge wa Uhuru
Historia ya nchi yetu ni pana na ya kuvutia kwa namna ya pekee ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika na Duniani kote. Upekee huu unatokana na uwezo wa kujenga hoja na uadilifu wa viongozi wetu, hasa mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipochaguliwa kuwa mjumbe kwenye Baraza la kikoloni la kutunga Sheria (Tanganyika Legislative Council) mwaka 1958.
Kwa kuwa Mwalimu alikuwa na ndoto ya kuiona Tanganyika na Afrika iliyo huru, mwaka 1958 katika hotuba yake ya kwanza alitamka maneno ya kifalsafa kwa wajumbe na Spika wa Baraza la kikoloni la kutunga Sheria kwa kusema “Sisi tunataka Uhuru wa Tanganyika, Mkitupatia tutauwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje na mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.

Maneno haya aliyarudia tena mwaka 1959 alipohutubia kikao cha 35 cha Baraza la Umoja wa Mataifa kama Mbunge mwakilishi pekee wa Tanganyika.
Falsafa hiyo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni kiashiria kikubwa kwa Waingereza kwamba watu wa Tanganyika wamechoka kutawaliwa. Siku Tanganyika ilipopata Uhuru tarehe 09 Desemba, 1961. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliuwasha Mwenge wa Uhuru na akamkabidhi Luteni Alexander Ngwebe Nyirenda na kikosi cha Vijana wenzake wakaupeleka Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro.
Mwalimu wakati akitoa hotuba ya siku ya Uhuru; aliwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia kwa ujumla kwa kusema                               “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna  matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo jaa dharau”
Luteni Alexander Nyirenda akipandisha Bendera na Mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro usiku wa kuamkia tarehe 9 december, 1961           

Baada  ya  Uhuru wa Tanganyika na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru,  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kulijenga taifa huru la Tanganyika; kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano na kuweka sera za kukabili  maadui ujinga, umaskini na maradhi.
Awamu hii  ilitafsiri falsafa ya Mwalimu aliyoijenga katika Mwenge wa Uhuru kwa kuweka  misingi madhubuti ya uhusiano wa nje, sera ya kutofungamana na siasa za upande wowote, na kuweka msisitizo mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika na mapambano dhidi ya ubeberu na vibaraka wao. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha lililosisitiza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni matunda ya utelekezaji wa Falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
Mara baada  ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kupata Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mafanikio makubwa katika kutekeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwani Wazanzibar walirejeshewa matumaini yaliyokuwa yametoweka chini ya utawala wa Kisultani.
Hata baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, falsafa yaMwenge wa Uhuru iliendelezwa kwa kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujenga na kuimairisha misingi ya amani, umoja, uzalendo, upendo, mshikamano na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii zetu na kupeleka kwa Watanzania wote ujumbe maalum uliokusudiwa na Serikali kila mwaka. Aidha, Mwenge wa Uhuru ni chombo pekee tulichonacho kama taifa cha kuwaunganisha Watanzania na kuwa wamoja kwani haufungamani na itikadi za kisiasa, makabila yetu wala Dini zetu. Mwenge wa Uhuru ni mali ya Watanzania wote.
Kwa nini Mwenge wa Uhuru husimamiwa na Serikali
Hadi mwaka 1992, Mbio za Mwenge wa Uhuru zilikuwa zikisimamiwa na kuratibiwa na Chama Tawala.   Baada ya nchi yetu kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992; mwaka 1993 Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza kusimamiwa na Serikali chini ya Wizara yenye dhamana na Maendeleo ya Vijana.  Mabadiliko hayo yalikuwa ni kiashiria kikubwa kwa watanzania wote kwamba Mwenge wa Uhuru hauna Chama, hauna kabila na hauna dini isipokuwa ni  kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa. Kwa sasa Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar. Aidha, rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa hutolewa na Serikali na hutengwa na Wizara zenye dhama na kupitishwa na Bunge la bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka wa fedha husika.
Tangu Mbio za Mwenge wa Uhuru ziasisiwe hadi leo, misingi na madhumuni ya Mwenge wa Uhuru na Mbio zake zimeendelea kuwa zenye manufaa makubwa na zitaendelea kurithishwa vizazi hadi vizazi katika taifa letu.

Rais wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na wawakilishi kutoka chama cha upinzani cha Chadema siku ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2013, sherehe zilizofanyika mkoani Iringa.
Faida na Mafanikio ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Kimataifa.
                     I.        Mwenge wa Uhuru umekuwa ni chombo muhimu cha kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi zetu za kisiasa, dini wala makabila yetu. Umuhimu huu unatokana na ukweli kwamba, leo hii tunahitaji kujenga Taifa lenye amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa kuliko wakati wowote ule ikiwa ni pamoja na kujenga taifa lisilokuwa na dhuluma, unyonge, rushwa, ubaguzi, ukabila, udini wala vitendo vya kifisadi.
                   II.        Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, Uvuvi  endelevu, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za jamii katika maeneo yote nchini na hasa katika maeneo yasiyofikika kiurahisi. Kwa mfano, kwa mwaka 2015 pekee, miradi 1,342 yenye thamani ya Tshs. 463,519,966,467.77 ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. Kati ya fedha hizo, Tshs. 73,462,492,473. 62 zilitokana na nguvu za wananchi.  Hata hivyo, michango yote inayotolewa na wananchi ni ya hiari na hutolewa baada ya wananchi kuhamasishwa na kufahamu umuhimu na matumizi yake ambayo ni kugharamia kwa miradi yao wenyewe.

                  III.        Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi katika maeneo yote nchini jinsi ya kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria na kupambana na matumizi ya Dawa za kulevya. Pamoja na njia nyingine tunazotumia kuwahamasisha wananchi wetu. Bado Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa ni njia sahihi ya kufikisha taarifa na elimu sahihi ya changomoto hizi kwa watanzania wote.
                 IV.        Mbio za Mwenge wa Uhuru pia, zimeendelea kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa watanzania wa pande zote mbili za nchi yetu.
                  V.        Kimataifa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana ya na maudhui yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu. Kwani umeendelea kuhamasisha amani ndani ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika na Duniani kwa ujumla. Tanzania imeendelea kuwa msuluhishi wa Amani Afrika na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine Duniani kote na imeshiriki ukombozi wa Bara la Afrika hasa kusini mwa Afrika na kusisitiza juu ya umoja, mshikamano, upendo na amani kwa mataifa hayo.
                 VI.        Mwenge wa uhuru umeendeleza falsafa ya kumulika ndani ya mipaka ya taifa letu kwa kumulika uovu katika jamii ikiwemo uzembe, kutowajibika, vitendo vya rushwa na ufisadi katika miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii nchini.
               VII.        Mbio za Mwenge wa Uhuru pia hutumika katika kuratibu na kutathimini shughuli mbambali za maendeleo zinazofanywa na wadau wa maendeleo na kukusanya taarifa zinazohusu kero za  wananchi ambazo husaidia Serikali katika upangaji na utelezaji wa mipango ya  maendeleo kwa wananchi wake.

Dhana Potofu dhidi ya Mwenge wa Uhuru.
Pamoja na maono ya Baba wa Taifa, falsafa ya Mwenge wa Uhuru , faida na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru ambao umeelezwa hapo juu, wapo watu wachache ambao huenda kwa sababu zao za kisiasa au maslahi yao binafsi wameamua kutumia nafasi zao na ushawishi wao kuupotosha umma wa Watanzania kwamba Mwenge wa Uhuru haufai kwa kutoa hoja  nyepesi (Cheap arguments). Hoja hizo hizo ni pamoja na:-
(i)      Falsafa ya Mwenge wa Uhuru haihitajiki sasa kwa Watanzania
Serikali kama ilivyoeleza hapo juu, inaendelea kusisitiza kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru na maono ya Baba wa Taifa juu ya taifa hili bado yanaendelea kuishi japo yeye hatupo naye tena kwani ni dhahiri kuwa chombo hiki kinasaidia sana katika jitihada za kuwaunganisha Watanzania, kujenga umoja wa kitaifa, upendo, mshikamano, amani, uzalendo na kuchochea shughuli za maendeleo kote nchini. Kwa sasa Mbio za Mwenge wa Uhuru zinahitajika zaidi kwa lengo la kuhamasisha watu wetu kufanya kazi na kujiletea Maendeleo kama silaha ya kupambana na adui ujinga na umaskini.

Picha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa anapokea Mwenge wa Uhuru




(ii)     Michango wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Serikali ingependa ifahamike kwa wananchi kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaendeshwa kwa rasilimali fedha za serikali zinazopitishwa na Bunge. Aidha, pale inapohitajika, wadau kwa hiari yao, husaidia katika kugharamia machapisho ya ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru uliokusudiwa kama jitihada zao katika kuisaidia Serikali kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi zaidi. 
Mbio hizi pamoja na dhana nyingine zilizofafanuliwa hapo awali, unawahamasisha wadau mbalimbali kushiriki na kuchangia kwa hiari shughuli za Maendeleo katika maeneo yao. Michango ya wadau katika Halmashauri zetu hujumuisha nguvu za wananchi, Vifaa na fedha taslimu ambazo hutumika katika miradi wanayoibuni na kuitekeleza wenyewe.  Lengo la kuwashirikisha wananchi katika miradi yao ya  maendeleo ni  kujenga  moyo wa kujitolea, uzalendo na utaifa kwa wananchi wetu ili  waweze kumiliki miradi inayoanzishwa na kujenga misingi ya uendelevu wa Miradi hiyo. Mara nyingi, asilimia ishirini ya kila mradi unaowekewa jiwe la msingi, kuzinduliwa, au kufunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ni sharti itokane na nguvu za wananchi. Serikali inaendelea kusisitiza kuwa, michango hiyo ni ya hiari na matumizi yake huwekwa wazi kwa wanachi kila mradi wakati wa kuzinduliwa au kuwekewa jiwe la msingi.
(iii) Mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na maambukizi ya VVU/UKIMWI
Baadhi ya watu wachache wamekuwa wakidai kuwa, mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru inachochea vitendo vya ngono zembe vinavyopelekea maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali inapenda kufafanua jambo hili kuwa, Suala la mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ni jambo linalopewa kipaumbele kikubwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Tangu mwaka 2000 hadi sasa, ujumbe wa mapambano dhidi ya UKIMWI umefanywa kuwa ujumbe wa kudumu na uandaliwa kwa kushirikiana na Tume ya taifa ya kuthibiti UKIMWI (TACAIDS) na kisha kutolewa kwa ufasaha na vijana wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa kila mwaka katika Halmashauri za Wilaya zote zote nchini. Lengo likiwa ni kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanafikia asilimia sifuri katika jamii yetu. Katika kufanikisha azma hii, Mbio za Mwenge wa Uhuru huwafikishia wananchi wote nchini, taarifa sahihi kukusu VVU/UKIMWI kwa njia ya machapisho, sanaa kama vile maigizo, mashahiri na nyimbo, ushuhuda (testimony) kutoka kwa waathirika na hotuba za wakimbiza Mwenge kitaifa ambao huandaliwa na mamlaka husika kabla ya kunza mbio hizi. Mbio za Mwenge wa Uhuru pia huhamasisha wananchi kupima VVU kwa hiari na kila siku, wastani wa watu 200 hadi 600 hujitokeza kupima VVU jambo ambalo ni nadra sana kutokea kwa watu wengi kujitokeza kupima VVU kwa wingi  katika program nyingine zinazolenga kuhamasisha upimaji wa VVU. Mbio za Mwenge wa Uhuru pia hukemea tabia za unyanyapaa katika jamii, huhamasisha juu ya matumizi sahihi ya ARVs na kuwaelekeza wananchi jinsi ya kujikinga na maabukizi ya VVU. Hivyo siyo kweli kuwa mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru inachangia katika maambukizi ya VVU. Ni vyema tukafahamu kuwa UKIMWI upo na tabia zetu hatarishi hasa za kufanya ngono zembe ndizo changamoto kubwa tunayotakiwa kuijadili kama Watanzania katika kupambana na ugonjwa huu wa UKIMWI na sio Mwenge wa Uhuru. Mwenge huu unatusaidia kupambana na tabia zetu hatarishi ambazo ndizo zimekuwa kikwazo kikubwa katika jitihada za Serikali za kupambana na VVU/UKIMWI.


Kutokana na umuhimu, dhana na falsafa ya Mwenge wa Uhuru kama ilivyoelezwa :-
·        Serikali itaendelea kujenga mshikamano, umoja, upendo na kudumisha amani miongoni mwa Watanzania kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru.
·        Serikali itaendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kuwahamasisha wananchi kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini kwa watu wetu.
·        Serikali itaendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kumulika, kufichua na kuchukua hatua dhidi ya watu au kundi la watu wanaojihusisha na vitendo vyote vinavyolihujumu Taifa ikiwa ni pamaoja na vitendo vya kibaguzi, rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe na chuki.

Serikali inapenda kutumia nafasi hii kuwaomba watanzania wote kutambua kuwa, kila taifa lina chimbuko lake, utamaduni wake, na taratibu zake. Mwenge wa Uhuru utabaki kuwa ni chombo muhimu na alama ya Taifa letu. Kama Taifa tutaendelea kushirikiana na kuenzi kazi na fikra za waasisi wa Taifa hili. Tushiriki katika shughuli za maendeleo kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru, tuusikilize ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unapopita katika maeneo yetu, tuutafakari na kuufanyia kazi kwa vitendo kwa maendeleo ya Taifa letu. Tujiepushe na biashara na matumizi ya Dawa za kulevya, vitendo vinavyosababisha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na tufanye kazi kwa bidii huku tukiendeleza mshikamo, umoja, upendo, amani na undugu wetu. Serikali inatoa wito kwa Vijana ambao ndiyo nguzo ya Taifa, kudumisha chombo hiki kwa faida yetu sote na vizazi vijavyo. Hapa Kazi tu.


Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Makala hii, imetolewa na:

Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

No comments