Header Ads

Profesa Muhongo Aichana Mikataba ya IPTL, Songas na Agreco........Asema Haina Tija Yoyote kwa Taifa


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mikataba yote ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni za kufua umeme siyo mizuri na haina manufaa yoyote kwa Taifa.

Profesa Muhongo alisema hayo juzi wakati akijibu hoja ya kuongezeka kwa deni la Tanesco iliyotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, John Mnyika.

Kambi ya upinzani imekuwa ikisema mikataba ya Tanesco haina tija kwa Taifa na imekuwa ikiliua shirika hilo. Katika hotuba yake, Mnyika alisema Tanesco imekuwa ikiilipa IPTL Sh300 milioni kwa siku kama gharama za uendeshaji.

Profesa Muhongo alikiri kwamba ni kweli deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu, rushwa, wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia.

Alisisitiza kwamba hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa.

“Lazima niseme ukweli, mikataba yote ya Tanesco siyo mizuri. Tumekuwa tukiwalipa Songas gharama za uendeshaji Dola 4.6 milioni; IPTL tunawalipa Dola 2.6 milioni; Agreco tunawalipa Dola 2.0 milioni. Hakuna mkataba wenye manufaa kwa Taifa,” alisema Profesa Muhongo na kuahidi kwamba wizara yake itachukua hatua ili kulinusuru shirika hilo na mzigo huo wa madeni kila mwezi.

Alisema wizara yake imeanza utaratibu wa kufanya tathmini ya utendaji wa wafanyakazi wa Tanesco ili kuhakikisha wanatoa huduma bora. 

Alisema tathmini hiyo inafanywa kwa mameneja wa Tanesco kwa kuangalia wameingiza kiasi gani na wameunganisha wateja wangapi.

“Kila baada ya miezi mitatu tunafanya tathmini ya mameneja wetu na mwezi wa sita tutafanya tathmini ya pili. Wapo ambao walishindwa kukidhi vigezo katika tathmini iliyopita, wameondolewa,” alisema waziri huyo.

Kuhusu suala la umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema Hazina imetoa Sh70.2 bilioni kwa ajili ya kumalizia utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa umeme vijijini, unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Jambo hili lililalamikiwa na wabunge wengi wakisema wakala huyo anashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu fedha zake hazitolewi na Serikali.

Walishauri fedha za Rea ziwekwe katika akaunti yake maalumu bila kupitia Hazina. Hata hivyo, Profesa Muhongo alilihakikishia Bunge kwamba miradi yote iliyobaki katika awamu ya pili ya Rea itakamilika kufikia mwisho wa mwezi ujao.

Alisema miradi ya Rea haitatetereka kwa sababu ya Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC) kusitisha kutoa misaada kwa Tanzania akisema Serikali imejipanga kusimamia miradi ya maendeleo bila kutegemea misaada ya wahisani.

“Tumeanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta (Pura). Wakala huyu atakuwa na jukumu la kusimamia mikataba yote ya mafuta na atasimamia pia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),”alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu suala la migodi kutolipa kodi, waziri huyo alisema ni kweli mingi hailipi na kusema ameanza kusimamia suala hilo na kuwa wote lazima walipe kodi.

Alisema Serikali pia itawalipa fidia wakazi wa Lindi katika eneo ambalo kitajengwa kiwanda cha kupakia gesi (LNG). Alisema fedha zipo na vijana wakasome Veta ili wapate ajira katika kiwanda hicho.

No comments