Header Ads

Nzega wahoji sukari kupanda kiholela

BAADHI ya wananchi wilayani Nzega mkoani Tabora wamelalamikia kupanda kwa bei ya sukari kutoka bei elekezi ya serikali ya Sh 2,000 kilo moja hadi kufikia bei ya Sh 2,500 hali iliyosababisha taharuki.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wilayani hapa kwa baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya jumla wanauza mfuko wa sukari wa kilo 25 kwa Sh 55,000 kutoka Sh 47,000, wa kilo 50 unauzwa Sh 110,000 kutoka Sh 97,000 hali inayowalazimu wafanyabiashara wa rejareja kuuza Sh 2,200, Sh 2,400 na wengine Sh 2,500 ili kupata faida kiasi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema kuwa mlipuko wa bei hiyo umewashtua hasa kwa kuchukua muda mfupi bila sababu ya msingi inayoeleweka.
Khadija Mambo alisema sukari itakuwa ikitumiwa na watu wenye kipato cha juu kutokana na wenye kipato cha chini kushindwa kumudu gharama hiyo ambayo imekuwa ikipanda siku hadi siku.
“Tumepata wakati mgumu sana na wengine sasa hatutatumia sukari kwani bei haieleweki na ni ya juu. Sisi watu wa daraja la chini haituimudu,” alisema Khadija akiwa dukani.
Shaaban Bundala alisema kwa sasa hakuna bei maalum inayoeleweka ya sukari kwani kila mfanyabiashara anauza kwa bei yake hali inayowachanganya wananchi na kujikuta wakishindwa kununua bidhaa hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa rejareja walithibitisha kupanda kwa bei ya sukari kwa madai ya kuwa maduka ya jumla yamepandisha bidhaa hiyo hivyo inawalazimu kupandisha ili kupata faida kidogo.
Oswadi Nation alisema si kwamba wanapenda faida kubwa, bali ni kutokana na mlipuko wa bei na kuiomba serikali isimamie maamuzi yake ya kuhakikisha bei ya sukari inaeleweka na kuepuka kupanda kiholela.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wameiomba serikali kufanya uchunguzi mkubwa na kubaini sababu za sukari kupanda na endapo ikabainika kuna uzembe hatua kali za kinidhamu zichukuliwe.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackline Liana alisema hatoweza kuzungumzia suala hilo kutokana na muda huo kuwa yuko katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Ofisa Biashara wa Wilaya, Leonard Luzilo alisema taarifa hizo za kupanda kwa sukari wameshazipata na kuzituma mkoani tayari kwa kupatiwa ufumbuzi dhidi ya kushusha bei. Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanapunguza bei ya sukari hadi kufikia bei elekezi ya serikali, na kuwaonya watakaokaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa haraka.

No comments