Header Ads

Mchungaji wa KKKT Aanguka na Kuzirai Kanisani Akibatiza Mtoto Wa Mchungaji Mwenzake

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Tumbi, David Bundi, ameanguka kanisani na kuzirai wakati akimbatiza mtoto wa mchungaji mwezake. 

Tukio hilo lilitokea jana wakati wa ibaada ya asubuhi katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kibwegere Kibamba, Dar es Salaam ambapo mchungaji huyo alikuwa amealikwa na mchungaji wa kanisa hilo, Margret Chekoloa. 

Mashuhuda wa tukio hilo, waliokuwa kanisani hapo walisema, Bundi baada ya kumaliza muda wa kusifu na kuabudu, ulifika wakati wa kubatiza, ambapo miongoni mwa watoto waliokuwa wakibatizwa alikuwamo wa Mchungaji Margret. 

“Kama unavyojua kanisani tulikuwa tumemaliza utaratibu wa kusifu na kuabudu, kilikuwa ni kipindi cha ubatizo na kati ya watoto waliokuwa wakibatizwa mmoja wapo ni mtoto wa mchungaji wetu Grace Denis. 
 

“Kitu kilichotokea ni baada tu ya mchungaji kupiga magoti na mtoto huyo kwa ajili ya kuanza kumbatiza alipoteza fahamu. 
 

“Hali hiyo ilizua taharuki kubwa miongoni mwa waumini wa kanisa hilo, hivyo ikabidi awahishwe Hospitali ya Theofilo iliyoko Mbezi kwa Msuguri, na kuacha zoezi la ubatizo likifanywa na mchungaji Margret ambaye alilazimika kumbatiza mtoto wake,” kilieleza chanzo hicho. 
 

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa mara baada ya kufanyiwa vipimo kwenye hospitali hiyo ilibainika kuwa mchungaji Bundi alikuwa na shinikizo la damu (presha) ambayo ilifikia 211 na hivyo kulazimika kuongezewa maji. 
 

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta mchungaji Margret kwa ajili ya kuelezea hali hiyo, lakini alikataa kuzungumza na kusema yeye hawezi kuongea lolote na badala yake atafutwe mtu mwingine anayeabudu kanisani hapo. 
 

“Siwezi kuongelea tukio hili, naomba uwatafute waumini wengine wa kanisa hili watakupa taarifa ila kwangu inakuwa ngumu kukwambia,” alisema Mchungaji Margret. 
 

Waumini wa kanisa hilo walisema kuwa hilo ni tukio la kwanza kutokea kanisani hapo, liliwapa wakati mgumu na kujikuta wakitoka nje kwa taharuki.
 
Chanzo-Mtanzania

No comments