Jeshi la Polisi lapewa siku 7 Liwe Limepeleka Mikataba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelipa siku saba kuanzia jana Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi, iliyopewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima.
Hadi sasa kampuni hiyo imeshalipwa asilimia 99 ya fedha, ilihali vituo vilivyofunga mashine hizo ni 14 kati ya 108.
Maagizo ya kamati hiyo yaliyotolewa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilal wakati kamati hiyo ilipokutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Aeshi alisema jeshi hilo mwaka 2011 liliingia mkataba na Kampuni ya Lugumi Enterprises kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima ambavyo viko 108.
Alisema mkataba huo ulikuwa wa Sh bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa kampuni hiyo imeshapewa asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo vilivyofungwa mashine hizo ni 14 tu, kati ya vituo vyote 108.
“Ukiangalia kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,” alisema Aeshi.
Kuhusu mali zinazokamatwa na polisi kwenye matukio mbalimbali nchini yakiwemo ya wizi, Kamati imewaagiza CAG, Polisi na Mhakiki Mali wa Serikali kufanya ukaguzi wa mali zote zinazokamatwa na polisi ili kuzifahamu kuzipa thamani halisi kulingana na idadi yake.
Alisema hivi sasa mali zinazokamatwa na polisi hazifanyiwi uhakiki kujua idadi na thamani yake hivyo nyingi zinapotea bila kujua zilipokwenda na nyingine ambazo kesi zake zimeisha, zinauzwa kwa bei ndogo kuliko thamani halisi.
Kuhusu maduka ya bidhaa ya majeshi nchini, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeiomba serikali idhini ya ukaguzi na utoaji mizigo ya maduka ya jeshi bandarini ufanywe na jeshi hilo badala ya utaratibu wa sasa ambao mzabuni ndiye anayesimamia jambo hilo.
Akizungumzia hilo, Aeshi alisema maombi hayo ya jeshi yalitolewa wakati kamati hiyo ilipokutana na JWTZ juzi na kuomba ukaguzi wa bidhaa zinazoagizwa kwa ajili ya maduka yao zifanyiwe ukaguzi na wao kwani inawezekana bidhaa zinazoingizwa zikawa nyingi au zikachanganywa na vitu vingine kwa kuwa wao hawana dhamana ya kukagua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa nyumba na kwamba mikakati yao hivi sasa ni kufanya mabadiliko na kulifanya jeshi hilo liwe la kisasa zaidi.
Post a Comment