Waziri Mkuu: Usalama Wa Chakula Umeimarika Nchini
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usalama wa chakula nchini
imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula.
Aliyasema
hayo jana (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa
hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa
hadi Aprili 3, mwaka huu.
Waziri
Mkuu alitaja mazao hayo kuwa ni pamoja na mahindi yaliyovunwa katika
mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa.
“Matarajio
yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri kwa sababu mwenendo wa
unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi
nchini.”
Alisema
Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na
usalama wa chakula unaendelea kuwa imara kwa wananchi wote na kwa
wakati wote.
Waziri
Mkuu alisema Serikali inawezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula
kuendelea kusafirisha na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi.
Hivyo,
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima waendelee
kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao stahiki
na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa
mavuno.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema upatikanaji na usambazaji wa
pembejeo kwa wakulima umeimarika, ambapo takwimu zinaonesha kwamba hadi
kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbolea nchini kwa ajili ya
mahindi na tumbaku ulifikia tani 250,376 sawa na asilimia 51.6 ya
wastani wa mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka.
“Katika
kipindi hicho hicho, mbolea za kupandia na kukuzia zipatazo tani
229,839 ziliingizwa nchini na kusambazwa mikoani. Upatikanaji wa dawa za
maji na unga (Salfa) kwa ajili ya mazao ya pamba na korosho
unaendelea.”
Waziri
Mkuu alisema hadi kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbegu bora
nchini ulifikia tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji halisi
ya tani 60,000 kwa mwaka. Katika kipindi hicho jumla ya tani 22,357 za
mbegu bora zilisambazwa nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Post a Comment