Serikali kuwashughulikia Polisi wanaotesa raia wakiwa kizuizini
Serikali
imeahidi kuwashughulikia Askari Polisi watakao bainika kutesa na
kuwapiga raia wakiwa kizuizini, kwa kuwa vitendo hivyo ni kinyume na
sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kifungu cha 11.
Kauli
hiyo imetolewa jana Februari 10, 2018 Bungeni mjini Dodoma na Naibu
Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad Masauni wakati
akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Rungwe (Chadema) Sofia Mwakagenda
lilohoji kama kuna sheria inayomruhusu Askari Polisi kumkamata mtuhumiwa
na kumpiga na kumtesa kabla ya kufikisha kituo cha polisi.
Eng.
Masauni alisema serikali kupitia wizara yake imekuwa ikiwachukulia
hatua Askari Polisi wanaofanya makosa mbalimbali, ambapo katika kipindi
cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2017, jumla ya askari polisi 105
waliotenda makosa mbalimbali wamechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa
pamoja na kufukuzwa kazi.
“Kwa
mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura 20 kifungu 11
kinaeleza namna ya ukamataji, aidha kifungu hiki mahsusi cha ukamataji
hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia akiwa kizuizuni, kwa mujibu
wa kanuni za utendaji wa jeshi la polisi askari yeyote atakayebainika
kutesa, kupiga raia akiwa kizuizini huchukuliwa hatua za kinidhamu
ikiwemo kufukuzwa kazi au kufikishwa mahakamani,” alisema.
Post a Comment