Header Ads

Wabunge Wataka Wapewe Ulinzi, Serikali Yagoma

Bunge limeagiza Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ifanyiwe marekebisho ili kuweka sharti la wabunge kupatiwa ulinzi, hususan katika makazi yao wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kibunge mjini Dodoma na katika maeneo yao ya uwakilishi.

Chombo hicho cha kutunga sheria pia kimeagiza kuweka utaratibu wa kutoa namba maalum za usajili wa magari ya wabunge huku kikiitaka serikali iboreshe na kuimarisha ulinzi katika maegesho ya magari bungeni.

Hayo yalisema na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, alipowasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati kwa kipindi cha Februari, 2017 hadi Januari, 2018.

Agizo hilo limetoka ikiwa ni takribani miezi minane tangu kushambuliwa kwa kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alipigwa risasi akiwa anajiandaa kushuka kwenye gari lake nyumbani kwake Area D mjini hapa Septemba 7, mwaka jana.

Mpaka sasa, hakuna taarifa ya kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo na Lissu anaendelea na awamu ya tatu ya matibabu yake ya kibingwa nchini Ubelgiji.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, Spika Job Ndugai aliiagiza kamati hiyo kulifanyia kazi na kulitolea taarifa bungeni.

Balozi Adadi alisema katika kipindi cha Novemba mwaka jana, kamati yake ilipokea na kujadili taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu udhibiti wa usalama wa viongozi wakiwamo wabunge.

Alisema uchambuzi wao ulibaini viongozi wanaolindwa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria ni viongozi wakuu wa nchi ambao ni Rais na Makamu wa Rais wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na viongozi wakuu wastaafu.

Alisema wengine ni viongozi waandamizi wa serikali ambao ni mawaziri na manaibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na Spika na Naibu Spika wa Bunge.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hupewa ulinzi wa jumla wanapokuwa katika shughuli za bungeni au kwenye safari zao za kikazi," Balozi Adadi alisema na kuongeza:

"Utaratibu huu unaliacha suala la ulinzi na usalama wa wabunge katika makazi yao wakiwa kwenye shughuli za Bunge na kwenye maeneo yao ya uwakilishi kuwa jukumu la mbunge mwenyewe."

Balozi Adadi alisema kazi za wabunge katika kuisimamia serikali zinagusa maslahi ya watu au makundi binafsi ambayo yanaweza kujenga chuki dhidi yao.

Majibu ya Serikali
Katika majibu yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema wazo hilo ni zuri lakini nchi inatakiwa kuwekeza kwanza katika kuimarisha miundombinu kabla ya kutoa ulinzi kwa mbunge mmoja mmoja.

Aliongeza kuwa bila kuwa na miundimbinu mizuri, askari watakaopewa jukumu la kuwalinda watunga sheria hao watakuwa kwenye hatari kubwa ya kudhurika na hata kushambuliwa.

Mauaji Kibiti
Alisema kamati yake ilikutana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Septemba na Januari na ikaridhishwa na juhudi za serikali katika kushughulikia matukio mbalimbali ya uhalifu hususani matukio ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji yaliyohusisha mauaji ya viongozi, askari polisi, na raia.

"Nafurahi kutoa taarifa kuwa, kwa kazi nzuri iliyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo hayo, hali ya usalama sasa ni shwari.

Lakini kamati inasisitiza kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha kiini cha mauaji hayo kinajulikana na kudhibitiwa ili mauaji ya aina hiyo yasijirudie tena nchini," alisema.

Msongamano wa Wafungwa
Balozi Adadi pia alisema kamati yake imebaini kuna msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani nchini kutokana na kile ilichoona matumizi hafifu ya sheria zinazoruhusu adhabu mbadala kwa wafungwa kama vile kifungo cha nje na mahabusu kutopelekwa mahakamani kwa muda uliopangwa.

Pia kutotumika ipasavyo kwa mpango wa Parole, kasi ndogo ya kusikiliza mashauri yanayohusu mauaji na dawa za kulevya pamoja na kutokutekelezwa kwa adhabu iliyotolewa dhidi ya wafungwa waliohukumiwa kunyongwa.

"Hali hiyo inaathiri afya za wafungwa na mahabusu. Vilevile, kuiongezea serikali gharama za kuwatunza," alisema.

Ajali
Alibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Desemba, jumla ya ajali 1,428 ziliripotiwa na kati yake, ajali 562 zilisababisha vifo.

Alisema idadi hiyo ya vifo ni pungufu kwa vifo 91 kulinganishwa na idadi ya vifo vya aina hiyo katika kipindi kama hicho mwaka 2016.

Alisema vifo vingi vya ajali vinachangiwa hasa na mwendokasi, kutovaa kofia ngumu, kutofunga mikanda, matumizi ya vilezi, matumizi ya simu za mikononi na matumizi ya vizuizi vya watoto.

Balozi
Mkurugenzi huyo wa zamani wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) pia alisema kamati yake imebaini uchakavu wa majengo ya balozi za Tanzania kutokana na kutofanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.

Pia alizungumzia changamoyo ya meli zenye usajili Tanzania kukamatwa nje ya nchi kwa makosa ya kihalifu ambayo ni pamoja na kubeba dawa za kulevya na vifaa vya kutengenezea silaha kali za kivita.

Alisema kamati yake inaishauri serikali kuchukua hatua za haraka kama ilivyoahidi mbele bungeni Mei 2, mwaka jana.

Utekaji na Amri za Wakuu wa Wilaya
Balozi Adadi pia alisema kamati yake ilibaini kumekuwa na ucheleweshaji wa kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu hatua zilizofikiwa katika upelelezi wa matukio ya muda mrefu na yanayovuta hisia za jamii kama vile matukio ya mauaji, kutekwa na kupotea kwa viongozi na wananchi mbalimbali, unyang'anyi wa kutumia silaha na makosa makubwa ya uhujumu uchumi.

"Kamati pia ilibaini kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya wanawaweka mahabusu wananchi na watumishi wa umma kinyume cha matakwa ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1997," alisema.

"Ni wajibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Tamisemi kuendelea kuwaelimisha wakuu wa wilaya kuhusu matumizi sahihi ya sheria hiyo ingawa kwa sasa vitendo hivyo vimepungua."

Credit: Nipashe

No comments