Header Ads

GODBLESS LEMA AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI BAADA YA KUTOKA MAHABUSU

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo imemuachia kwa dhamana Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya kuwa amekaa mahabusu kwa miezi minne.
Godbless Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana ambapo mara kadhaa maombi ya dhamana yake yalikwama mahakamani na kumlazimu kuendelea kukaa mahabusu kwa muda wote huo.
Lema anakabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya Rais Dkt Magufuli kufuatia maneno aliyoyatoa akiwa bungeni mjini Dodoma.
Baada ya kutoka leo, Lema amepata muda mfupi wa kuzungumza na waandishi wa habari ambapo amesema;
“Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Jamhuri ilikusudia mabaya kwangu lakini Mungu alikusudia mema kwetu, vilevile namshukuru sana mke wangu, kama ningepata fursa ya kuoa tena ningemuoa yeye.. Nikisema niongee ninachotaka kuongea, leo sitaweza, nimeandaa waraka kwa ajili ya mheshimiwa Rais na nitautoa huo waraka hivi karibuni katika siku ambayo tutawatangazia. Nimeona mateso mengi ya watu, mambo mengi ambayo nafasi hii haitoshi.”
Mbunge huyo ameachiwa leo baada ya kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili na kusaini bondi ya TZS milioni moja.

No comments