Trump atangaza kujenga kinu kikubwa cha silaha za nyuklia Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuwa anataka kujenga kinu kikubwa cha nyuklia nchini humo kuhakikisha kuwa taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani linaendelea kuwa juu zaidi katika silaha za nyuklia.
Akizungumza leo katika mahojiano maalum na shirika la habari la Reuters, Rais Trump amesema kuwa Marekani sasa hivi iko nyuma katika uwezo wake wa silaha za atomiki.
Katika hatua nyingine, Reuters imemnukuu Trump akizungumza baada ya mahojiano hayo, ambapo alieleza kuwa anachukizwa sana na kitendo cha Korea Kaskazini kufanya majaribio ya silaha zake za maangamizi.
Alisema kuwa katika kuidhibiti Korea Kaskazini, Marekani inapaswa kutumia mfumo wa nchi marafiki kama Japani na Korea Kusini.
Ni nchi tisa pekee duniani zilizothibitisha kuwa na silaha za kinyuklia ambazo ni Urusi, Marekani, China, India, Israel, Ufaransa, Korea Kaskazini, Pakistan na Uingereza. Nchi nyingine zinazodaiwa kuwa na silaha hizo zimekua zikikanusha vikali na kudai kuwa zinatumia nyuklia kama nishati.
Kwa mujibu wa shirika linalojihusisha na masuala ya usalama, Ploughshares Fund, linakadiria kuwa kuna zaidi ya silaha za nyuklia 15,000 duniani kote, ambapo Marekani na Urusi pekee zinamiliki zaidi ya asilimia 93 ya silaha hizo.
Post a Comment