Header Ads

Rais Magufuli awapongeza madaktari Muhimbili na amsaidia Neema Mwita Wambura aliyeunguzwa moto kifuani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Neema Mwita Wambura ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.

Pongezi hizo za Mhe. Dkt. Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema Mwita Waitara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa maendeleo ya afya yake.

Katika Pongezi hizo Mhe. Dkt. Magufuli amesema Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na ambayo yalitishia uhai wake.

Pia Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mama Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa upendo wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake huko Tandika Devis Kona Jijini Dar es Salaam.

“Nakushukuru sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kabla ya kutoa pongezi hizo, mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amewatuma wasaidizi wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa kwenda Tandika Devis Kona katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam kumuona Neema Mwita Wambura ambaye alipatiwa hifadhi katika nyumba ya Mama Mjane aitwaye Mariam Amir (Bibi Mwanja) baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika mitandao ya kijamii.

Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi laki 5 kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia chakula yeye na watoto wake waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda Mkoani Mara na pia ametoa Shilingi laki 5 kwa Mariam Amir aliyejitolea kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake. Pia ameahidi kumsaidia wakati wote wa matibabu na pia familia yake.

Baada ya kumpokea daktari bingwa wa magonjwa ya dharula na ajali katika kitengo cha dharula cha Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga amesema wameanza kumfanyia uchunguzi ili kujua maendeleo yake na kama kumpa matibabu zaidi.

Nae Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma ambaye amekuwa akimfanyia matibabu Neema Mwita Wambura tangu Julai 2015 alipofikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza amesema Neema anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji mara nne.

Dkt. Mkoma amesema baada ya upasuaji huo, sasa Neema anaweza kuinua na kugeuza shingo yake na kwamba kwa sasa wataendelea kumfanyia uchunguzi zaidi ili kujua maendeleo yake. Mhe. Rais Magufuli ameagiza vyombo vyote vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema Mwita Wambura na kuhakikisha haki inatendeka.



No comments