KUKANUSHA TAARIFA ZA UZUSHI KUHUSU AFYA YA MZEE MWINYI
Kumekuwa na
habari zinazoenea na kujirudia sana katika mitandao ya kijamii kuhusu hali ya
afya ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Alli Hassan Mwinyi. Taarifa hizo
ambazo hazieleweki lengo lake, zimekuwa zikidai kuwa Mzee Mwinyi amefariki
dunia.
Tunautaarifu
umma kuwa habari hizo si za kweli, ni za kupuuzwa. Mzee Mwinyi ni mzima wa
afya, anaendelea na majukumu yake kama kawaida ambapo jana Alhamisi amehudhuria
chakula cha jioni kuadhimisha siku ya Taifa la Kuwait na leo mchana alitarajiwa
kwenda kumjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya.
Natumia fursa
hii kuendelea kuwakumbusha watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa waliobuni
teknolojia hii walikuwa na malengo adhimu ya kumpatia mwanadamu uwanja na
uwanda mpana wa mawasiliano-tusiwachezee shere wabunifu hao kwa kuitumia
kinyume cha malengo.
Aidha, jamii
ifahamu kuwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya
Mitandaoni, 2015, kwa mtu yeyote kutangaza, kuchapisha au kueneza habari za
uongo au uzushi katika mitandao.
Kwa niaba ya Serikali nachukua fursa hii kuwapa pole
familia ya Mzee Mwinyi na watanzania wengine kwa mshtuko walioupata kutokana na
uzushi huu. Katika hili hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
watakaobainika kuhusika na uhalifu huu.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa
Serikali
Post a Comment