BABA AMJERUHI VIBAYA MWANAYE KWA KUMTAHIRI KWA KISU....APATA ULEMAVU KWA KUKATWA KIPANDE KIKUBWA CHA UUME
MKAZI wa Kijiji cha Mihingo wilayani Bunda mkoani Mara, Marwa Elias (28) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda kwa tuhuma ya kumtahiri vibaya kwa kutumia kisu, kukata kipande kikubwa cha uume wa mtoto huyo na kumsababishia madhara makubwa mwilini mwake.
Mtoto huyo mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mihingo, amefanyiwa ukatili huo na mwanaume huyo, na kumsababishia ulemavu huo. Kwa sasa mtoto huyo anajisaidia haja ndogo kwa shida huku akisikia maumivu makali kutokana na kukatwa sehemu hiyo ya siri vibaya.
Elias alifikishwa katika mahakama hiyo na kushitakiwa kwa kosa la kumfanyia madhara makubwa mwilini mtoto huyo.
Mwendesha mashitaka wa Polisi, Masoud Mohamed, alisema kuwa mtu huyo anatuhumiwa kutenda kosa hilo Aprili 10, mwaka jana, saa nne asubuhi katika eneo la kijiji hicho kinyume cha sheria.
Mohamed alidai mbele ya Hakimu Abelina Kashushura kuwa mtuhumiwa huyo, alitenda kosa hilo wakati akimtahiri kwa kutumia kisu mwanafunzi huyo wakiwa nyumbani kwa mtoto huyo katika kijiji hicho cha Mihingo.
Ilidaiwa kuwa wakati mwanaume huyo akiendelea na kazi hiyo, alimjeruhi vibaya mwanafunzi huyo (jina lake limehifadhiwa) kwa kumkata sehemu kubwa isivyo kawaida ya eneo hilo. Aidha, ilidaiwa kuwa baada ya tendo hilo, mtuhumiwa huyo alitoweka na kwenda kwenye shughuli zake, akimuacha mtoto huyo akiwa na hali hiyo.
Kwamba, baadaye hivi karibuni alikamatwa na kufikishwa polisi na kisha mahakamani hapo.
Baada ya kusomewa shitaka lake mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na kupelekwa mahabusu katika gereza la Nyasura, nje kidogo ya mji wa Bunda, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 23 mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya mjini Bunda, Abelina Kashushura, kutokana na mahakimu wa mahakama ya wilaya hiyo, kutokuwepo siku hiyo mahakamani hapo kwa sababu ya kuwa dharura.
IMEANDIKWA NA AHMED MAKONGO-HABARILEO BUNDA
Post a Comment