Dk. Mbassa wa Chadema afariki dunia akiwa usingizini
ALIYEKUWA Mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Anthony Mbassa alifariki dunia jana usiku akiwa usingizini nyumbani kwake.
Taarifa zilizopatikana kutoka Biharamulo na kuthibitishwa na Msemaji wa familia, Pendo Ngonyani, zilieleza kuwa kifo cha Dk. Mbassa kilifahamika alfajiri ya jana.
Alisema watoto walipokwenda kumuamsha hakuamka hali iliyowalazimu kumuita mama yao ambaye aliwasiliana na madaktari wa Hospitali ya Biharamulo na kuthibitishwa kuwa alikuwa amefariki dunia.
Dk. Mbasa ambaye alikuwa mbunge mwaka 2010 baada ya kushinda uchaguzi mkuu, hakurejea kwenye ubunge baada ya kuangushwa na mshindani wake, Oscar Mkasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.
Akizungumzia kifo hicho, Pendo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kagera, alisema Dk. Mbassa alifariki dunia akiwa usingizini.
Pendo alisema haijafahamika sababu ya kifo chake ingawa familia imedokeza inataka uchunguzi ufanyike kubaini sababu ya kifo hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, juzi mkewe akiwa kazini, yeye (Dk. Mbasa) alitoka na kurudi jioni saa 12 na kuacha gari lake nyumbani na kwenda ambako hakujajulikana. Alirudi nyumbani saa 5.00 usiku akiwa akionekana kuwa amelewa.
“Nimeelezwa kuwa baada ya kuacha gari alitoka kwa mguu kuanzia hiyo saa 12 na kurejea yumbani saa 5.00 usiku. Haijajulikana alikwenda wapi lakini alirejea akiwa amekunywa alikuwa akihangaika na ilidhaniwa ni hali ya pombe, ndiyo hivyo asubuhi alikutwa akiwa amefariki dunia.
“Leo alikuwa na safari ya kwenda Bukoba kuwasiliana na mawakili wake kwa ajili ya kushughulikia madai ya fidia ya Sh milioni 60 za gharama za kesi namba 5/2010, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo hilo, Oscar Mkasa,” alisema.
Alisema kinachosubiriwa hivi sasa ni ndugu na jamaa kupanga utaratibu wa maziko.
Post a Comment