Header Ads

WAGANGA WA TIBA ASILIA BUKOMBE WAPITISHA KATIBA YAO.

                          Mkuu wa Wilaya Bukombe Aman Mwenegoha


NA MAKUNGA MAKUNGA,
BUKOMBE

 UMOJA wa waganga wa tiba asilia wilayani Bukombe Mkoani Geita jana wamepitisha Katiba yao itakayowaongoza katika kusimamia na kutekeleza shughuli zao wanazozifanya kila siku ili kujenga umoja na mshikamano na kubaini waganga makanjanja wanaopiga Ramli chonganishi zinazopelekea mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi ALBINO.

Mwenyekiti wa umoja huo Mohamed Masupura aliwataka waganga wote wahakikishe wanailinda na kuitetea katiba hiyo kwani ndani yake inakataa kabisa upigaji wa Ramli chonganishi.
Masupura aliwashukuru waganga wenzake kwa ushirikiano wao ambao wameuonesha kati yao na Serikali Wilayani hapa kwani kwa ushirikiano huo mauaji ya vikongwe yamepungua. 

Mkuu wa wilaya bukombe Amani Mwenegoha akiwa mgeni Rasmi na msimamizi wa hafla amewapongeza waganga hao kwa kushirikiana na serikali katika kuwabaini na kuwafichua waganga uchwara ambao hufika na kutundika vitambaa na kuanza kutibu kwa umoja wao wakomeshe vitendo hivyo.
Pia mwenegoha amewapongeza kwa kuunda katiba yao na kuwa na vibali vya tiba toka kwa mratibu wa tiba asilia anayetambulika kisheria toka Hospitali ya Wilaya ambaye ni Dr Luzeke Mbogo ambaye atawaelimisha na kuwaongoza hadi kwa mkemia mkuu ili wapate ushauri wa jinsi ya kufunga dawa zao kwenye vifungashio vya kisasa.
Mwenegoha amewaeleza waganga hao kuwa kwa sasa jamii inahitaji kupata dawa zilizofungwa kama vidonge , za maji zifungwe kwenye chupa kama juisi sanjari na dawa zile za unga wa poda ziwekwe kwenye makopo na zipimwe na kuwekewa muda wa mwisho wa matumizi bila kusahau kuweka bayana madhara yake.
Pamoja na hayo mkuu huyo ametoa wito kwa waganga wa tiba asilia wote wilayani hapa wahakikishe wanapendana na kuthaminiana na kuhakikisha waganga wote wanajiunga na umoja huo kwani tayari kila kijiji na kitongoji kina uongozi.
Mwisho amewataka wahakikishe kuwa mauaji ya vikongwe yanakoma na hayatokei katika maeneo yao, ili kujilinda na kuendelea kuheshimiwa kwa kazi yao hiyo ya mizimu ambayo ilikuwepo kabla hata ya kuwepo kwa Dini ya aina yeyote katika Tanzania na Afrika yote.

No comments