Header Ads

Maalim Seif Asema Hakuna Ajenda Yoyote Ya Kisiasa Waliyozungumza Na Dr. Shein Ambaye Alimtembelea Juzi Serena Hoteli Kumjulia Hali


Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema mikutano yake ya hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein haikuwa na agenda yoyote ya kujadili hali ya kisiasa inayoendelea visiwani Zanzibar.

Maelezo hayo ya Maalim Seif yanamaliza minong’ono iliyopo nchini baada ya kutembelewa na Rais John Magufuli na baadaye siku hiyohiyo na Rais Shein na kuzusha hisia kuwa huenda kulikuwa na jambo zito la kisiasa hasa ikizingatiwa kwamba zilikuwa zimebaki siku takriban 10 kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo ambao kiongozi huyo wa upinzani ametangaza kwamba hatashiriki.

Maalim Seif aliwaambia wanahabari jana kuwa Dk Shein alikwenda kumjulia hali kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli na watu wengine wenye mapenzi mema, hivyo hakuna haja kwa Wazanzibari kuwa na hofu yoyote.

“Tusingeweza kuzungumza lolote wakati afya yangu siyo nzuri sana. Unapozungumza mambo mazito kama hayo ya uchaguzi lazima uwe mzima kimwili na kiakili,” alisema Maalim Seif baada ya kujuliwa hali na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Maalim ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka jana alisusia uchaguzi huo wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha baada ya kuufuta wa awali kutokana na kuvunjwa kwa taratibu na sheria.

Msimamo huo ulipigiliwa misumari na Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililoeleza kuwa chama hicho hakitashiriki uchaguzi huo na kuitaka ZEC iondoe majina ya wagombea wote wa chama hicho katika karatasi za kupigia kura.

Mbali na CUF, uchaguzi wa marudio umesusiwa na vyama vya upinzani takriban 10 licha ya ZEC kusisitiza kuwa haitaondoa majina kwa kuwa taratibu za kisheria za kujiondoa hazikufuatwa.

Maalim Seif amepumzika katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam baada ya kutoka katika Hospitali ya Hindu Mandal ambako alilazwa kwa matibabu mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza hotelini hapo jana, Lowassa alisema alikwenda kumjulia hali Maalim Seif na ameridhika kuona afya yake inazidi kuimarika.

Pia, mazungumzo yao na Lowassa ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita aligombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, hakuyahusisha masuala ya siasa wala uchaguzi huo wa marudio wa visiwani humo.

No comments