Header Ads

Mzee Afia Kwenye Choo cha Msikiti Visiwani Pemba



MTU mmoja mwenye umri wa miaka 80 amekutwa akiwa amefariki  ndani ya choo cha  msikiti wa Ibadhi ulioko Bopwe  karibu na Ofisi za Baraza la Wawakilishi Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini Kwake , Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamishina msaidizi Hassan Nassir Ali alisema  aliyefikwa na mauti hayo ni Hassan Ali Juma mkaazi wa Bopwe Wete .

Alisema  mzee huyo aliondoka nyumbane kwake  machi 9 majira ya saa saba , kuelekea msikitini kwa ajili ya maandalizi ya swala  ya adhuhuri , na kuonekana machi 10 majira ya saa 12.45 jioni akiwa amefariki ndani ya choo .

Inadaiwa  kuwa  mzee huyo baada ya kufika msikitini  aliingia chooni kisha kufunga mlango kwa ndani ambapo alianguka akiwa katika harakati za kufua fulana alilokuwa amevaa  ili aoge.

“Tumebaini kwamba mzee huyo alianguka katika harakati za kuvua fulana , ambapo tumemkuta akiwa amefunikwa na fulana usoni huku akionekana kuumia zaidi sehemu za kichwani ”alifahamisha .

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jina wa jeshi la Polisi Mkoa Issa Juma Suleiman  aliwataka wananchi kutoa taarifa katika jeshi la Polisi wanapopotelewa na jamaa zao ili wasaidiane kuwatafuta .

Alieleza kwamba tangu mzee huyo alipopotea hakuna mtu aliyefika na kutoa taarifa katika jeshi la Polisi jambo ambalo ni kinyume na utaratibu .

Naye mdogo wa marehemu Khamis Ali Juma (42) alisema kabla ya kufikwa na mauti hayo kaka yake hakuwa na matatizo yoyote kiafya , na aliondoka nyumbani kwa ajili ya kuwahi swala ya Adhuhuri katika mskiti wa Ibadhi .

Mashuhuda wa tukio hilo walifahamisha baada ya kuona mlango umefungwa walichungulia na kumuoa akiwa amelala chini , ndipo juhudi za kuvunja zilichukuliwa chini ya usimamizi wa jeshi la Polisi .

No comments